Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAPA NA PALE

HAPA NA PALE

UM umetangaza kuwa sasa hivi unaweza kuthibitisha kihakika kwamba maiti 17 zimeonekana karibu na eneo lilipotukia ajali ya ndege iliokodiwa na UM , nje ya mji wa Bukavu, katika mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo JKK). UM unajitayarisha, kwa sasa, kuendeleza shughuli za kuchunguza utambulisho wa mabaki ya maiti. Miongoni mwa waathiriwa hao walikuwemo raia wanne wa Kongo pamoja na raia mmoja wa Kanada, watumishi wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP).

Mawaziri wa afya wa kutoka eneo la Afrika kusini ya Sahara - linalojulikana kama ‘ukanda ulioselelea maradhi ya uti wa mgongo’ - waliokusanyika Yaoundé, Cameroon kwenye mkutano ulioungwa mkono na UM, Alkhamisi wametoa mwito ulioahidi kutengeneza chanjo mpya ambayo wanatumai itasaidia kuwakinga watu milioni 250 dhidi ya ugonjwa huo maututi. Ahadi inayojulikana kama Mwito wa Yaoundé, inawakilisha mradi mpya wa pamoja kudhibiti maradhi ya uti wa mgongo, unaojumuisha huduma za kuimarisha mawasiliano juu ya namna ya kudhibiti janga hili kidharura, na taratibu za kufadhilia shughuli za kukinga umma na maradhi. Mwito wa Yaoundé umekusudiwa kuyahudumia mataifa 25 afya bora, kwenye eneo la ‘ukanda wa maradhi ya uti wa mgongo’, uliosambaa kuanzia Senegal, Afrika Magharibi hadi Ethiopia, katika mashariki ya Afrika, maeneo ambayo, katika siku za nyuma, yalighumiwa na mifumko ya mara kwa mara ya homa maututi ya uti wa mgongo.

Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imekataa kuiridhia rufaa iliokatwa na mwendesha mashtaka ya kupinga uamuzi wa kabla wa Jaji kusitisha kesi ya aliyekuwa kiongozi wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Thomas Lubanga Dyilo, ambaye alituhumwa kuajiri watoto walio na umri mdogo kushiriki kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Mnao Juni 13, 2008 Mahakama ya ICC ilipitisha amri ya kusitisha kwa muda utekelezaji wa hukumu ya kumwachia Lubanga baada ya kugundulikana waendesha mashtaka walibania nyaraka 200 na kumnyima wakili mtetezi, nyaraka ambazo zilijumlisha ushahidi uliokuwa na uwezo wa kuthibitisha kihakika kwamba mtuhumiwa Lubanga alikuwa hana hatia na makosa aliyoshtakiwa.

Shirika laUM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti kuwa Ijumanne ya tarehe 02 Septemba, kwenye kambi ya wahamiaji Darfur, kulizuka fujo ya chakula iliosababisha kifo kwa mtu mmoja na watu sita wengineo kujeruhiwa, ikijumuisha polisi watatu. Tukio hili lilijiri katika kambi ya Um Shalaya, iliopo kilomita 70 kusini-mashariki ya El Geneina, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Magharibi, ambapo idadi kubwa ya wahamiaji wakazi hao huwa wanatokea taifa jirani la Chad. Fujo zilianzishwa saa nne asubuhi pale mamia ya wanawake na akina mama waliochukua fimbo walianza kuandamana kwa kelele na ghadhabu, wakilalamika kupunguziwa posho ya mtama. UNHCR ililazimika kupunguza posho hiyo, kwa muda, kwa sababu ya upungufu wa akiba ya chakula kwenye ghala zake kutokana na mashambulio ya yale malori yaliokodiwa na UM yanayogawa chakula katika maeneo ya wahamiaji. Kwenye kambi ya Um Shalaya wanaishi wahamiaji 6,600 katika mazingira ambayo, kila mwezi, hufura wahamiaji ziada wanaomiminikia huko kutokea Chad mashiriki kukwepa mapigano kwenye maeneo yao.