Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alkhamisi (04/09/08) alasiri Baraza la Usalama limepitisha taarifa mbili, moja ikisisitiza kwamba kunazingatiwa, kwa uangavu mkubwa, na wajumbe wa Baraza ile rai ya kupeleka vikosi vya ulinzi amani, vya kimataifa, Usomali katika siku za usoni kuchukua nafasi ya majeshi ya Umoja wa Afrika yaliopo huko hivi sasa. Kadhalika, taarifa iliyakaribisha mazungumzo, ya kiwango cha juu, ya kuunganisha tena taifa liliogawanywa miaka ya nyuma la Cyprus, baina ya raia wa Kigiriki na wale wa Kituruki.

Shirika la Wahamaji wa Kimataifa (IOM) limetangaza idadi ya wahamaji wa ndani wanaorejea kwenye miji ya Baghdad na Diyala imeongezeka katika siku za karibuni, kutokana na kinyanyua mgongo cha fedha wanachofadhiliwa na Serikali ya Iraq, na pia kuambatana na madai ya usalama kurejea tena kwenye eno. Kadhalika wenye madaraka Baghdad wametangaza kuanzisha operesheni za kuwang’oa watu waliojikalia kimabavu kwenye nyumba ambazo wenyewe walihama mastakimu kidharura kutokana na vurugu la kimadhehebu liliotanda nchini Iraq kwa muda.

Mkutano wa kila mwaka wa Idara ya Habari ya UM (DPI) pamoja na mashirika yasio ya kiserikali (NGOs)umekamilisha mijadala yake leo Ijumaa mjini Paris, Ufaransa. Hii ni mara ya kwanza kikao cha DPI/NGOs kufanyika mbali na Makao Makuu ya UM ya New York. Mada za mkutano wa safari hii zililenga kwenye masuala yanayohusu haki za binadamu.