UM umeitisha mjadala maalumu kusikiliza hisia na maoni ya waathiriwa wa ugaidi duniani
Hii leo, kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, kumeanzishwa mjadala maalumu wa kihistoria, ulioandaliwa na KM Ban Ki-moon mwenyewe, ambao umewakusanyisha waathiriwa wa vitendo vya ugaidi kutoka sehemu kadha za kimataifa na kuwapatia fursa ya kuelezea hisia zao juu ya misiba waliopitia, kwa madhumuni ya kuwakilisha taswira ya kiutu kwa waathiriwa wa janga la ugaidi duniani.
Kwenye hotuba ya ufunguzi mkutanoni, KM Ban Ki-moon alieleza kwamba kikao kimeitishwa kwa makusudio ya kuonyesha “ushikamano wa jumuiya ya kimataifa na waathiriwa wa maafa ya ugaidi ulimwenguni”, na “kwa ajili ya utu unaotuunganisha wanadamu wote, tumelazimika kuandaa jukwaa la kimataifa” aliongeza kusema KM, kusikiliza sauti za waathiriwa wa janga ovu na katili la ugaidi. Majadiliano yaliendelea kwa siku nzima.