Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAPA NA PALE

HAPA NA PALE

Naibu KM Asha-Rose Migiro ameondoka New York Ijumatano kuelekea Lebanon kuhudhuria kikao cha 12 kilichotayarishwa na Baraza la Maendeleo ya Uchumi na Jamii kwa Asia ya Magharibi (ECOWAS) kitakachokutana kuanzia Septemba 13 hadi 14, 2008. Madhumuni ya mkutano ni kushauriana namna ya kusawazisha shughuli za mashirika ya UM ili kuimarisha mshikamano, kukuza ushirikiano na kujiepusha na tabia ya kurudufia kazi zao.

UM umeomba msaada wa dola milioni 108, kwa niaba ya Haiti, utakaotumiwa kuwahudumia watu 800,000, sawa na asilimia 10 ya idadi ya watu nchini, ambao wameathirika vibaya sana na madhara ya vimbunga vitatu vilivyopiga taifa hiklo kwa mfululizo katika wiki za karibuni. Inakadiriwa watu 70,000 sasa hivi wanaishi kwenye makazi ya muda, na takriban sehemu zote za kilimo zimefurika maji, ikimaanisha mavuno yote ama yameharibika sana au yameshaangamia. Msaada wa kimataifa ukifadhiliwa utawapatia waathiriwa hao, katika miezi sita ijayo, huduma za msingi za kiutu pamoja na misaada ya mapema inayohitajika kufufua shughuli za maisha ya kawaida.