Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

UM na mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu, yanayosimamia huduma za kuendeleza ilimu kwenye maeneo ya mgogoro Usomali, yametoa taarifa yenye kulaani vikali mashambulio ya karibuni dhidi ya majengo ya skuli, walimu na wanafunzi yaliofanyika katika mji wa Mogadishu.

Shirika la Ulinzi Amani kwa Darfur la Mchanganyiko wa Vikosi vya UM/UA (UNAMID) limeripoti Ijumatano kwamba moja ya lori lao linalotumiwa kuzoa maji machafu ya majumbani lilitekwa nyara na watu wenye silaha, kwenye eneo la kilomita 2.5 kutokea kambi ya wahamiaji ya Zamzam. Kwa mujibu wa ripoti za UNAMID watu watatu waliokuwa na silaha walilijongelea lori la UNAMID na kumlenga dereva, na kumlazimisha alisogeze gari kuelekea Kambi ya Wahamiaji wa Ndani ya Zamzam na kutoroka nalo. UNAMID imo mbioni kujaribu kulipata lori lao.

Alkhamisi msafara wa kwanza wa UM, uliobeba shehena ya misaada ya kiutu, uliruhusiwa kuingia kweneye eneo la Gori kaskazini linalodhibitiwa sasa hivi na vikosi vya Kirusi, na kujaribu kuzipatia aila zilioathirika na uhasama wa karibuni mahitaji ya kimsingi. Katika jaribio la kwanza la kupeleka misaada hiyo kwenye eneo husika, misafara ya UM ilishindwa kuingia katika kituo cha ukaguzi cha Karaleti. Tani nne za misaada ya kihali zilipelekwa kwenye kijiji cha Patara Garadjivari ambapo wakazi wa huko waliomba wapatiwe ulinzi bora, makazi yanayofaa, chakula na huduma za afya.

Wakuu wa mashirika ya UM yenye Makao Makuu Roma, Utaliana ambayo hushughulikia misaada ya chakula, yaani mashirika ya miradi ya chakula duniani, WFP; chakula na kilimo, FAO na mfuko wa maendeleo ya kilimo, IFAD walipata fursa ya kuhutubia Kamati juu ya Maendeleo ya Bunge la Ulaya na kuitaka taasisi hiyo kuwafadhilia wakulima wa nchi zinazoendelea, msaada wa uro bilioni moja, fedha ambazo hazijatumiwa na kikawaida hupatiwa msaada wakulima wao. Waliinasihi Kamati hiyo kutekeleza pendekezo lao wenyewe aslia ambalo ilitaka kuziweka fedha hizo kwenye mfuko maalumu utakaotumiwa baadaye kupiga vita njaa na upungufu wa chakula kwenye mataifa masikini. Wakurugenzi wa mashirika matatu hayo ya UM walikumbusha kwamba wakulima maskini katika nchi zinazoendelea, kwa sasa, wamekosa uwezo wa kupandisha mbegu kondeni mwao kwa sababu hawamudu tena kununua mbegu na mbolea na wanahitajia misaada ya kimataifa.

Mkataba muhimu wa kimataifa, unaojulikana rasmi kama Mkataba wa Cartagena juu ya Usalama wa Viumbe Hai, leo umeadhimisha miaka mitano tangu ulipoidhinishwa na kuwa sheria ya kimataifa. Mkataba huu umedhamiriwa kuhakikisha taaluma ya kisasa juu ya tafiti za viumbe hai inakuzwa na kuendelezwa kwenye mazingira yalio salama. Kadhalika Mkataba unalenga kuimarisha usalama kwenye usafirishaji, utunzaji na matumizi ya viumbe hai vilivyobadilishwa kitaaluma (yaani kadhia ya Viumbe Vilivyogeuzwa kwa Vinasaba – GMO). Hadi sasa, nchi 147 na Jumuiya ya Ulaya zimeshaidhinisha au kuridhia Mkataba huo.