Srgjan Kerim ana matumaini mema juu ya mageuzi katika BU

17 Septemba 2008

Raisi aliyepita wa kikao cha 62 cha Baraza Kuu, Srgjan Kerim, ambaye alimaliza muda wake Ijumatatu, (15/09/08) alipokutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu hapo jana, alibainisha ya kuwa kulipatikana mafanikio makubwa kwenye kazi za Baraza, chini ya uongozi wake, hasa pale wajumbe wa kimataifa waliporidhia kuzingatia uwezekano wa kurekibisha na kuleta mageuzi kwenye mfumo wa Baraza la Usalama.

Kadhalika, alisema maafikiano yanayohusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani, na maamuzi ya kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi na zile za kiraia kukabiliana na suala hili, ni makubaliano ya kikao cha 62 yenye kuashiria hatua muhimu kwenye juhudi za kuhifadhi mazingira, kwa ujumla. Halkadhalika, Raisi aliyepita wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim alisema kikao kilichomalizika Ijumatatu kimefanikiwa “kufanya maandalizi yanayoridhisha” kuhusu ule mkutano wa vyeo vya juu, utakaofanyika tarehe 25 Septemba ambapo viongozi wa kimataifa watajumuika Makao Makuu, pamoja na wawakilishi wa sekta ya binafsi na jumuiya za kiraia, na kusailia taratibu za kuchukuliwa kwa pamoja kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa wakati katika nchi husika.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter