Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapitio ya majadiliano ya jumla katika kikao cha 63 cha Baraza Kuu

Mapitio ya majadiliano ya jumla katika kikao cha 63 cha Baraza Kuu

Mnamo siku ya tatu, na ya nne, ya majadiliano ya wawakilishi wote kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la UM, ambayo yalifanyika Alkhamisi na Ijumaa, wingi wa viongozi wa kutoka Afrika, hususan wale waliowakilisha mataifa ya kusini ya Sahara, walishtumu na kulaumu juu ya namna mifumko ya bei za chakula na nishati kwenye soko la kimataifa zilivyoathiri na kuhariibu shughuli zao za kiuchumi na jamii.~

Raisi Robert Mugabe wa Zimbabwe yeye alisema kwenye risala yake ni muhimu kuhakikisha juhudi za kitaifa za kukabiliana na mizozo ya chakula na nishati huwa zinakamilishwa kwa hatua ziada, zinazofaa, za kimataifa, ikijumlisha lilependekezo la kufuta madeni yanayodaiwa nchi zenye mapato madogo na zenye upungufu wa chakula. Alisema Zimbabwe ina imani kubwa kuhusu maadili ya taasisi yenye wahusika wingi wa kimataifa, mathalan, UM; walakini, wakati huo huo, alisema angelipendelea kuona demokrasia zaidi inajumuishwa kwenye shughuli za UM yenyewe kwa sababu mfumo uliopo hivi sasa, alisisitiza, hutumiwa na mataifa yenye nguvu kwenye Baraza la Usalama lenye wajumbe 15, “kama jukwaa la kuhalalisha, kwa urahisi, majungu na njama zao za kisiasa.”

Mfalme Mswati III wa Swaziland alilalama bei ya juu ya chakula na nishati hukoroga zaidi shinikizo za matatizo yanayoyavaa nchi maskini yanayochochewa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, janga la UKIMWI/VVU na maradhi mengine yanayozuilika kama malaria na kifua kikuu. Hata hivyo alitiwa matumaini kuwa UM haijayapuuza mataifa haya, hususan yale mashirika yake yanayojihusiha maendeleo ya kilimo na chakula (FAO) na miradi ya chakula duniani (WFP), ambayo bado “yanaendelea kuzisaidia nchi hizo kutafuta suluhu ya kudumu kukomesha mzozo wa chakula kwenye maeneo yao.”

Raisi James Alix Michel wa Ushelisheli aliliambia Baraza Kuu mfumo wa udanganyifu wa biashara katika soko la kimataifa ndio unaozorotisha na kukwamisha maendeleo na alisihi jumuiya ya kimataifa kusita kutumia “suluhu inayoendelea kutajirisha zaidi matajiri na kufukarisha na kuwafanya kuwa maskini zaidi walio dhaifu.” Alisema ruzuku wanaopatiwa wakulima wa nchi tajiri, zenye maendeleo ya viwandani, huyanyima mataifa yanayoendelea uwezo halali wa kuuza bidhaa zao kwa bei ya mghalaba kwenye soko la dunia. Wakati huo huo nchi maskini zinatarajiwa kisheria kufuata kikamilifu kanuni za Shirika la Biashara Duniani (WTO), hata ikiwa sheria hizo “hukandamiza sera za uchumi wa kizalendo zilizobuniwa kuhifadhi na kuwalinda raia maalhakiri, walio dhaifu kijamii.”

Jens Stoltenberg, Waziri Mkuu wa Norway alipohutubia ukumbi wa Baraza Kuu Alkhamisi usiku alishtumu ya kwamba kutofaulu kwa walimwengu kwenye zile juhudi za kupunguza, na kudhibiti vifo vya uzazi, ni ushahidi kamili wenye kuthibitisha dharau ziliopo katika maamirisho ya maendeleo kwa wanawake. Alikumbusha kwamba udhibiti wa vifo vya watoto wachanga na uzazi bora ni miongoni mwa yale Malengo ya Milenia muhimu yanayohitajia kukamilishwa kwa wakati, ili kusukuma mbele ustawi wa jamii. Alilaumu mapuuza dhidi ya maendeleo ya wanawake yanasabibishwa na hali ya ulimwengu uliotawaliwa na kuongozwa na wanaume. Alipendekeza kuwepo mfumo madhubuti utakaoiwezesha jumuiya ya kimataifa kutumia fedha zaidi kuimarisha mahitaji ya maendeleo kwa wanawake. Alitaka kuongezwe majengo ya skuli Afghanistna, fedha maridhawa kuhudumia hospitali Rwanda na kuhakikisha kuwa wakazi wa mitaa ya mabanda huwa wanapatiwa chanjo kinga dhidi ya maradhi yanayozuilika.

Waziri wa Masuala ya Kimataifa na Ulaya wa Shirikisho la Austria, Ursula Plassnik naye vile vile alishiriki kwenye majadiliano ya jumla kwenye Baraza Kuu, ambapo risala yake iliwazindua wawakilishi wa kimataifa kuhusu janga karaha la udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsiya. Alisema matumizi ya mabavu na nguvu dhidi ya wanawake ni vitendo vinavyolazimika na kuwajibika kuvikomesha, halan, kote ulimwenguni. Alipendekeza kuwepo malengo, yenye uwazi, ya kusitisha janga hili na kuanzisha mtandao wa kimataifa utakayoyasaidia Mataifa Wanachama kubadilishana mawazo juu ya taratibu madhubuti za kufuatwa kuyatekeleza hayo.

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown alihutubia mjadala wa UM Ijumaa ambapo alitoa mwito unaogftaka kuanzishwe mfumo mpya wa fedha wa kimataifa, utakaokomesha mtafaruku wa kiuchumi ulioupamba ulimwengu sasa hivi. Alisema tunaishi kwenye mazingira ya ulimwengu uliojaa khitilafu zenye kugongana, maana kwa upande mmoja tunashuhudia kipindi chenye mafanikio na ustawi mkuu wa kutia moyo, na kwa muda huo vile vile tunaendelea kujikuta kwenye enzi ya ulimwengu uliojaa mitafaruku, vurugu na zahama. Alikumbusha kwamba ni wajibu wa kimataifa kukomesha tabia ya kutojali mahitaji ya umma; na alipendekeza kukuza ushirikiano utakaojenga “mfumo mpya wa kimataifa wa fedha utakaokuwa na uwazi, kinyume na ule mfumo wa usiri na ufichaji; utaratibu ambao hutuza mafanikio, na sio ubadhirifu uliopindukia; utaratibu wenye majukumu ya kudhaminika na sio ile tabia ya kupona adhabu; mfumo wenye natija kimataifa na sio kitaifa pekee.”

Waziri Mkuu wa Uholanzi, Jan Peter Balkenende, kwenye hotuba alioiwasilisha katika mahojiano ya jumla ya Baraza Kuu alihimiza kusarifiwe mazungumzo miongoni mwa jamii mbalimbali zenye kufuata itikadi za dini, imani na maadili tofauti, ili kukuza tabia ya kuhishimiana kitamaduni, utaratibu ambao, alitilia mkazo, ni muhimu kuendelezwa kwenye jamii za kisasa zenye asili tofauti. Alisema kila serikali ulimwenguni hukabiliwa na ubishi mkubwa katika kusawazisha mahitaji ya maadili ya kitamaduni na kidini na mila za raia wake, na huwajibika kujenga daraja za ufahamiano wenye natija kwa umma wote wa kimataifa.

Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nchi za Nje wa San Marino, Fiorenzo Stolfi alisema kwenye risala yake mbele ya Baraza Kuu kwamba ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kuwa na mazungumzo ya pamoja yenye dhamira ya kukuza uelewano miongoni mwa tamaduni na itikadi za dini tofauti, kwa sababu mwelekeo kama huo katika uhusiano wa kimataifa, alisistiza, unalingana na kuthibitisha kihakika miongozo ya maadili ya Umoja wa Mataifa.

Mwana atakayerithi Ufalme wa Brunei, Haji Hassanal Bolkiah Mu’izzadin Waddaulah alikumbusha kwenye taarifa yake mbele ya Baraza Kuu kwamba taifa lake, kwa muda mrefu lilikuwa kwenye msitari wa mbele kuunga mkono ile rai ya kufanyisha mazungumzo ya kukuza uelewano miongoni mwa jamii zenye dini tofauti, ili kuimarisha hali ya kuvumiliana na kufahamiana kitamaduni.