Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhakika wa majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

Uhakika wa majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu

Ijumaa wingi wa viongozi wa dunia, kwenye majadiliano ya wawakilishi wote yaliofanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu, yalioingia siku ya tano, walikubaliana juu ya umuhimu wa kuikabidhi UM madaraka ya kusimamia juhudi za kusuluhisha mizozo iliojiri hivi sasa kwenye soko la kimataifa, kuhusu mifumko ya bei za chakula na kupanda kwa kasi kwa bei za nishati pamoja na matatizo ya fedha katika soko la kimataifa.

Waziri Mkuu wa Bara Hindi Manmohan Singh aliposhiriki kwenye majadiliano ya Baraza Kuu alikiri kwenye hotuba yake kwamba jumuiya ya kimataifa inahitajia kuchukua hatua za dharura kuweza kukabiliana na matatizo yanayolingana ya chakula na nishati, na kukabili pia vurugu la mzozo wa fedha uliozuka kwenye soko la kimataifa. Alipendekeza UM utumiwe kuwa ndio chombo muhimu cha kimataifa, chenye uwezo wa kuongoza ushirikiano unaojumuisha Mataifa yote Wanachama, pindi shughuli zake zitarekibishwa na kuhuishwa ili kuwasilisha matokeo yanayotarajiwa. Aliyataka Mataifa kutekeleza ahadi zilizotolewa 2005 za kuleta “mageuzi yenye maana kwenye Baraza Kuu, mapema iwezekanavyo” na alitumai taasisi hiyo itaendelea kufanywa kuwa ni chombo kikuu cha kushauriana kimataifa. Wakati huo huo Waziri Mkuuwa Bara Hindi alitaka kupatikane marekibisho kwenye mfumo wa Baraza la Usalama ili uwakilishe hali halisi ya karne ya ishirini na moja.

Raisi FilipVujanović wa Montenegro alikubaliana na msimamo wa Bara Hindi na alisisitiza kwenye hotuba yake kwamba UM ndio wenye mfumo imara wa kuimarisha demokrasia, na kutunza haki za binadamu, pamoja na kuhakiksiha sheria ya kimataifa inahishimiwa na maendeleo ya kiuchumi na jamii yanakuzwa kwa natija za wote. Alikumbusha kwamba msingi wa maadili yanayoongoza shughuli za UM yanatilia mkazo umuhimu na ulazima wa ushirikiano wa wahusika wingi.

Gabriel Ntisezerana, Naibu Raisi wa Pili wa Burundi hotuba yake ilizingatia zaidi mafanikio ya kidemokrasia nchini na kuomba msaada wa kimataifa uongezwe kuimarisha maendeleo hayo. Alisema katika 2005 Burundi ilibahatika kuanzisha taasisi za kidemokrasia nchini, na zilizochaguliwa kwa utaratibu wa kidemokrasia, hali ambayo, kwa mara ya kwanza, iliwezesha matokeo ya uchaguzi nchini kuhishimiwa na raia kwa miaka mitatu mfululizo, na katika wakati ambao, hatimaye, umma wa Burundi nao uliweza kustarehea matunda ya kumalizika kwa vita nchini.

Abbas El Fassi, Waziri Mkuu wa Morocco taarifa yake kwenye mahojiano ya Baraza Kuu ililaumu kwamba licha ya kuwa juhudi kadha wa kadha ziliwakilishwa kwenye mikutano ya UM zilizohimiza misaada rasmi ya maendeleo ifadhiliwe kidharura nchi maskini, katika miaka michache iliopita misaada hiyo ilionekana kuporomoka kwa kima kinachoshtusha. Alisema misaada haba iliotolewa na wahisani wa kimataifa haikufanikiwa kukidhi mahitaji ya nchi zinazoendelea, licha ya kuwa nchi tajiri ziliahidi kukuza msaada huo kila mwaka, hadi dola bilioni 50 itakapofika 2010. Hali hii, alitilia mkazo, ndio iliosababisha nchi kadha katika Afrika kutota kwenye rika ya mataifa yasioendelea.i Mkuu wa Morocco alipendekeza kwa UM kujihusisha zaidi kwenye huduma za kuyasaidia mataifa maskini kujikomboa kutoka mazingira ya ufukara na hali duni.