Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ndege ya helikopta iliokodiwa na UM kuhudumia Vikosi vya Mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) iliripotiwa kuanguka na kuharibiwa kabisa ilipoanza kuruka kutoka Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini. Wahudumu wanne wa helikopta hiyo walifariki. Marie Okabe, msemaji mshiriki wa KM, aliwaambia waandishi habari ya kwamba ripoti za awali zilizopokewa na UM zimethibitisha ndege yote iliteketea. Taarifa ziada zinatarajiwa kutangazwa baada ya UNAMID kumaliza uchunguzi kamili kuhusu ajali.~

Kwenye kikao cha Mkutano wa Mawaziri uliofanyika New York kuzingatia utekelezaji wa Mpango wa Utendaji wa Brussels, Naibu KM Asha-Rose Migiro aliwakumbusha washiriki wa mkusanyiko huo ya kwamba wamebakiza miaka miwili tu kabla ya kumaliza utekelezaji wa ahadi walizotoa juu ya mradi muhimu wa miaka 10 wa kupiga vita ufukara, pamoja na kukabiliana na mifumko ya bei za chakula na bei za mafuta ya petroli, na kudhibiti athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi maskini. Kikao kilijumuisha hasa wawakilishi wa kutoka mataifa yanayoendelea. Miongoni mwa mambo yalioahidiwa kutekelezwa na Mpango wa Utendaji wa Brussels ilikuwa ni pamoja na kuendeleza utawala bora kwa nchi maskini, na mataifa tajiri yalitakiwa kutumia baina ya asilimia 0.15 hadi 0.2 ya pato la jumla la taifa kufadhilia maendeleo ya nchi zinazoendelea.

Mgogoro wa afya Uchina uliochochewa na maziwa ya unga yaliosibika na kiwango kikubwa cha kemikali ijulikanayo kama melamine, umelilazimisha Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa mwongozo wa awali wa dharura kuwasaidia wenye madaraka kuamua vipimo vinavyofaa kuingizwa kwenye chakula. Kwa mujibu wa taarifa za UM watoto 54,000 waliotumia maziwa ya unga yenye melamin katika Uchina walihitajia kupata matibabu baada ya kuripotiwa walikutikana vijiwe kwenye mafigo yao. Ripoti ilisema watoto 13,000 waathiriwa walilazwa hospitali baada ya kunywa maziwa yenye melamin, na watoto watatu waliripotiwa kufariki kwa sababu ya maradhi ya figo. WHO inasema kemikali ya melamin ilitiwa kwa miezi kadha, kwenye maziwa yasiopikwa, kwa makusudio ya kuongeza nguvu ya protini.