Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za UM mipakani Ethiopia na Eritrea zasitishwa

Operesheni za UM mipakani Ethiopia na Eritrea zasitishwa

Shirika la Kusimamia Ulinzi wa Amani Mipakani Ethiopia/Eritrea, yaani Shirika la UNMEE, limekomesha operesheni zake zote kwenye eneo kuanzia saa sita usiku Alkhamisi, kwa kufuatana na pendekezo la azimio 1827 (2008) la Baraza la Usalama, ambalo lilipitishwa, bila kupingwa, mnamo Ijumatano ya Julai 29 (2008).

KM alisema amesikitishwa na uamuzi wa makundi husika kukataa mapendekezo yake. Lakini alisema amekaribisha pendekezo la Baraza la Usalama la kumtaka aendelee kujihusisha na juhudi za kutafuta suluhu ya kurudisha utulivu na amani ya kudumu kieneo. Alitumai Ethiopia na Eritrea zitajitahidi kukwamua mzoroto uliojiri kwenye mzozo wao, na kujenga uhusiano mzuri kati yao, kitendo ambacho ndio kama ufunguo wa kuwasilisha amani na utulivu kwenye eneo lao. Alisisitiza KM kwamba yeye, binafsi, yupo tayari kutumia wadhifa wake kusaidia mataifa haya mawili kuharakisha utekelezaji wao wa Mapatano ya Amani ya Algiers.

Vikosi vya wanajeshi pamoja na watumishi raia wa UM waliotoka nchi 46, walishiriki kwa muda wa miaka saba ziada kulitumikia Shirika la UNMEE. Hivi sasa watu zaidi ya wafanyakazi 700 wa UNMEE bado wamesalia kwenye eneo kukamilisha shughuli zao. Wanajeshi 320 na watumishi raia 130 wapo katika upande wa mpaka, ndani ya Ethiopia, na watumishi raia 250 wamebakia ndani ya Eritrea.