Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Baada ya ziara ya siku tatu katika Msumbiji, Ann Veneman, Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) alitangaza kutolewa mchango wa dola milioni 3 ziada kusaidia ile mipango ya kuwalisha watoto nchini humo.

Inakadiriwa na takwimu za UM asilimia 41 ya watoto wadogo Msumbiji wanasumbuliwa na tatizo la utapiamlo. Veneman alikumbusha yakwamba licha ya kupatikana maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliojiri Msumbiji katika kipindi cha karibuni, hali ambayo imelisaidia taifa kuelekea kwenye mkondo wa kuyafikia Malengo ya Milenia (MDGs) kwa wakati, hasa katika kupunguza vifo vya watoto wachanga na vifo vya uzazi, hata hivyo, kutokana na mfumko wa bei za chakula kwenye soko la kimataifa na kitaifa, ikichanganyika na janga la UKIMWI, alitilia mkazo, ni hali ya mkorogano wa maaafa unaohatarisha maendeleo, kwa ujumla, nchini.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah ametoa taarifa maalumu yenye kudhihirisha masikitiko yake makubwa juu ya vifo vilivyotukia mwisho wa wiki iliopita, vya wanawake 20 wa Kisomali, kutokana na bomu liliotegwa ardhini mjini Mogadishu. Alisema hakuna "hoja yeyote ile inayohalalisha vifo vya watu wasio hatia". Ould-Abdallah alikumbusha "wanawake hao waliuawa wakati wakiendeleza kazi tukufu ya kutakasa maisha kwa kuusafisha mji mkuu wao wa Mogadishu." Aliwapelekea aila ya waathiriwa, wakijumuika na umma wote wa Usomali, mkono wa taazia na kuwataka "wazalendo halisi wa Usomali" kuvumiliana na kujitahidi kutatua matatizo yao kwa mazungumzo na kushauriana, kama ilivyowaidhiwa na dini pamoja na utamaduni wao wa jadi.