Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kimataifa juu ya UKIMWI umeanza rasmi Mexico

Mkutano wa kimataifa juu ya UKIMWI umeanza rasmi Mexico

Mkutano Mkuu wa XVII wa Kimataifa juu ya UKIMWI umeanza rasmi Ijumapili katika Mexico City, Mexico. Mkutano Mkuu juu ya UKIMWI hufanyika kila baada ya miaka miwili, na kikao cha 2008 cha Mexico kimehukusanyisha watu 25,000 wakiwemo wanasayansi, wawakilishi wa serikali, wahudumia afya, wanaharakati wanaopigania kufyeka janga la UKIMWI, na vile vile wagonjwa na watu wenye virusi vya UKIMWI.

Kwenye hotuba ya ufunguzi, alioitoa KM Ban Ki-moon Ijumapili, mbele ya wajumbe waliohudhuria Mkutano, aliyahimiza Mataifa Wanachama kuongeza juhudi zote muhimu zinazohitajika kulishughulikia suala hili kwa mafanikio, hasa ilivyokuwa bado nchi nyingi sana zimezorota, na ziko mbali sana katika kuyafikia yale Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yanayohusiana na huduma za kukomesha kabisa na kupunguza miripuko ya maambukizo ya UKIMWI itakapofika 2015.

KM alisema katika miaka ijayo kutahitajika mchango maridhawa wa kimataifa kuweza kukabiliana, kama inavyostahiki, na janga la UKIMWI hasa ilivyokuwa wagonjwa wingi walioambukizwa na VVU/UKIMWI hivi sasa humudu kupatiwa dawa za kurefusha maisha, hali yenye kumaanisha wanahitajia misaada ziada ya kudhibiti bora afya yao. Kadhalika, KM alipongeza kwenye risala yake sheria mpya iliopitishwa karibuni Marekani ya kuweka kando dola bilioni 48 kupiga vita UKIMWI, kifua kikuu na malaria kote duniani katika miaka mitano ijayo; na KM vile vile alizipongeza nchi wanachama wa Kundi la G8, yaani yale mataifa yenye maendeleo ya viwandani, kwa kuahidi kuongeza mchango wao wa kutumiwa kuzuia maambukizo ya UKIMWI na kusaidia kwenye huduma za matibabu ya maafa hayo ya kiafya itakapofikia 2010. Alitoa mwito kwa wanasiasa, kote ulimwenguni, kusaidia kukomesha ubaguzi na kutetea haki ya watu wanaoishi na kuathirika na virusi vya UKIMWI. Alipendekeza skuli nazo pia zichukue hatua za kufundisha tabia ya kuheshimiana na wagonjwa wa UKIMWI, na kuwataka viongozi wa kidini kuhubiri uvumilivu na waathiriwa wa magonjwa haya thakili, na wakati huo huo alivitaka vyombo vyote vya mawasiliano ya habari kuendelea kulaani aina zote za chuki zenye kudhuru hisia za kiutu dhidi ya wagonjwa wa maafa ya UKIMWI.

Peter Piot, Mkurugenzi wa Umoja wa Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) aliwaambia wajumbe waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa juu ya UKIMWI nchini Mexico mnamo Ijumapili usiku, ya kuwa, kwa mara ya kwanza, imeshuhudiwa na taasisi za UM kwamba ni watu wachache wanaofariki duniani siku hizi kutokana na maradhi ya UKIMWI, na vile vile kiwango cha watu wanaoambukizwa na UKIMWI kimeonekana kuteremka, halkadhalika. Matokeo haya, aliongeza kusema, ni ya kutia moyo, lakini si ya kujiridhisha wala ya kutangazia ushindi, maana masafa ya kuukomesha UKIMWI bado yapo mbali sana. Kwa hivyo, Piot alisema, kwa kurudia nasaha ya mwimbaji wa Visiwa vya Karibian, Bob Marley walimwengu wanajukumu la kukithirisha mchango wao kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI kama alivyohubiri msanii huyo ambaye alisema “Nyanyuka na usimame kidete … usisalim amri kamwe dhidi ya mapambano.”