Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Haile Menkerios, aliye Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa na pia Mjumbe Maalumu wa UM kwenye Kundi la Ushauri wa Upatanishi juu ya Zimbabwe, anaondoka New York leo Ijumanne (05/07/08) kuelekea Afrika Kusini, ambapo atakuwa na mazungumzo kuhusu maendeleo kwenye zile juhudi za kusuluhisha mvutano wa kisiasa Zimbabwe, ambazo zinasimamiwa na Afrika Kusini. Menkerios anatarajiwa kuzuru Zimbabwe baadaye kabla ya kurejea Makao Makuu mnamo mwisho wa wiki.

Ripoti mpya ya Shirika la UNICEF inayotathminia mwelekeo wa hali ya afya ya mama mzazi na watoto wachanga katika ukanda wa Asia na Pasifiki, kwa kufungamana na malengo ya nne na tano ya MDGs, imehitimisha kwa kusisitiza huduma hizo hazitofanikiwa kutekelezwa kwa wakati penye ukosefu wa afya bora kwa umma wa Bara Hindi na Uchina. Ripoti ilieleza kwamba Bara Hindi inahitajika kuonyesha maendeleo makubwa kwenye huduma za kuimarisha afya, lishe bora, usafi na maji salama, elimu ya msingi kwa wote, usawa wa kijinsiya na hifadhi ya watoto dhidi ya maambukizo ya maradhi. Kuhusu Uchina ripoti ilitilia mkazo umuhimu wa taifa hilo kudhibiti bora maendeleo yaliojiri siku za nyuma katika kuzuia vifo vya watoto wachanga.