Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya Mkutano wa XVII wa Kimataifa juu ya UKIMWI, 3-8 Agosti 2008, Mexico City, Mexico

Kumbukumbu ya Mkutano wa XVII wa Kimataifa juu ya UKIMWI, 3-8 Agosti 2008, Mexico City, Mexico

Taasisi ya Mfuko wa Kimataifa Kupiga Vita UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, ambayo hujulikana kwa umaarufu kama Global Fund, imetangaza Ijumatatu kwenye Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa XVII juu ya UKIMWI, unaofanyika Mexico City, Mexico ya kwamba mwaka huu imeshapokea maombi kutoka nchi 97 zinazotaka zifadhiliwe msaada wa fedha wa jumla ya dola bilioni 6.4 kukabilina na maradhi hayo matatu.

Taarifa ya Global Fund pia ilisema imethibitika kihakika, kwa mara ya kwanza ya kuwa zile nchi zilizoshiriki kwenye huduma kinga dhidi ya malaria, zilifanikiwa nazo pia kupunguza vifo vya watoto na maambukizi ya malaria kwa karibu asilimia 50, ikijumuisha nchi za Rwanda, Zanzibar, Eritrea, Burundi na baadhi ya sehemu za Msumbiji na Swaziland; wakati Ethiopia, Ghana, Kenya na Zambia nazo pia zilionyesha kupata mafanikio ya kutia moyo dhidi ya vifo vya malaria. Tangu Taasisi ya Global Fund ilipobuniwa katika 2002, imefanikiwa kuidhinisha msaada wa jumla ya dola bilioni 11.4 kwa nchi 136 ulimwenguni; taasisi hii hivi sasa ndiyo pekee kimataifa inayofadhilia robo moja ya misaada yote ya kupiga vita UKIMWI duniani, na vile vile hutoa thuluthi mbili ya misaada kuhudumia kifua kikuu, na robo tatu nyengine hutolewa kutumiwa kupambana na malaria katika sehemu kadha za kimataifa.

Kadhalika, Shirika la Afya Duniani (WHO) limechapisha na kuwasilisha kwenye Mkutano wa Kimataifa juu ya UKIMWI waraka mpya wenye lengo la kuyasaidia mataifa kukabiliana vyema zaidi na UKIMWI/VVU. Waraka huu unajumuisha furushi la maelezo muhimu ya kuzisaidia nchi zenye mapato wastani, na ya chini, kufikia, kwa urahisi, taarifa na ripoti zinazohusu huduma za kimataifa za kudhibiti bora hatari ya uenezaji wa UKIMWI/VVU, na pia kuyasaidia mataifa katika juhudi za uuguzi na kutibu wagonjwa waliopatwa na maradhi hayo. Furushi limekusanyisha mapendekezo muhimu yanayofahamisha namna ya kuingilia kati tiba ya udhibiti bora wa UKIMWI/VVU - kuanzia maelezo juu ya taratibu za kukithirisha matumizi ya mipira ya kondom kwenye jamii, pamoja na miongozo mengineyo yenye kuelezea taratibu mpya za kufuatiliwa, zinazotumia viwango vya kisasa katika kuuguza wagonjwa wenye UKIMWI/VVU. Waraka huu wa WHO umeandaliwa kuwa ni waraka ‘hai’ wa kwenye mtandao, na utakuwa ukirekibishwa mara kwa mara na ripoti mpya zitakazopendekeza matibabu ya UKIMWI/VVU yanayolingana na uzoefu unaoendelea kubadilika kiafya.