Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon amehuzunishwa sana na mapinduzi ya Serikali ya Raisi Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdallahi wa Mauritania yaliotukia 06 Agosti 2008 nchini humo. Kwenye taarifa iliotolewa Ijumatano juu ya tukio hilo KM alikumbusha ya kuwa serikali iliopinduliwa Mauritania ilichaguliwa kihalali mwezi Juni 2007, kwa utaratibu wa mfumo wa kidemokrasia wa vyama vyingi, na kwa hivyo alivinasihi vikundi vyote husika nchini humo kufuata sheria kwa kurudisha utulivu na amani na kufufua, halan, utaratibu wa katiba ya nchi.~

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM katika JKK ameripoti ataongeza juhudi zitakazohakikisha walinzi amani wa MONUC watafuata Kanuni za Kuendesha Kazi za UM na kupunguza tabia mbaya na vitendo karaha dhidi ya raia, vinavyokwenda kinyume na maadili ya Mkataba wa UM. Amesema ataanzisha tume ya hadhi ya juu ya wataalamu wa kitaifa, na kimataifa, watakaoisaidia MONUC kuhakikisha wanaoshiriki kwenye vitendo haramu watawajibika na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao kwa makosa hayo.

Kwenye risala alioituma KM tarehe 6 Agosti kwenye Taadhima ya Kumbukumbu za Amani za Hiroshima, Ujapani alisisitiza kwamba hisia za kimataifa kuhusu mahitaji ya kuwepo maendeleo halisi katika juhudi za kupunguza silaha za kinyuklia duniani, ni za nguvu zaidi katika kipindi cha sasa hivi, hasa ilivyokuwa makundi kadha wa kadha pamoja na watu binafsi wameonekana kupania vikali, sio kwa kauli tu bali pia kwa vitendo kutekeleza mradi wao. Alinasihi taadhima za Hiroshima zisifanyike kama ni jambo la ada ya mwaka tu, bali zitumiwe kama ni fursa ya kuuhamasisha umma wa kimataifa kuhishimu kumbukumbu ya waathiriwa wa kwanza wa vita vya atomiki, na wazingatie kinachohitajika kufanyika kuhakikisha tunakuwa na ulimwenngu ulionusurika na silaha za kinyuklia na amani ya kudumu.

Posta ya UM imetangaza kuwa itatoa stempu mpya sita za ukumbusho Ijumaa, tarehe 08 Agosti (2008) zitakazowakilisha “Amani kwenye Riadha” kwa kulingana na mwanzo wa mashindano ya michezo ya Olimpiki yatakayofanyika Beijing, Uchina. Picha za stempu hizo zilichorwa na msanii Romero Britto wa kutokea Amerika ya Kusini ambaye alijaribu kubainisha kwenye michoro yake maadili ya olimpiki ambapo halaiki ya umma wa kimataifa hujumuika kwenye mashindano ya riadha kwa amani.