Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM ameripoti kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa hali ya vurugu katika jimbo la Ossetia Kusini, Georgia. KM ameyanasihi makundi yote yanayozozana kwenye eneo hilo kujizuia kuchochea vitendo vitakavyopalilia uhasama na kuhatarisha utulivu wa eneo.~~

John Holmes, Naibu Katibu Mkuu juu ya Masuala ya Huduma za Dharura ameripoti kuwa ameshtushwa na kuongezeka kwa idadi ya raia wanaojeruhiwa kwenye ugomvi nchini Usomali. Alikumbusha ya kuwa ni wajibu kwa makundi yanayohasimiana Usomali, chini ya sheria ya kimataifa, kuwalinda na kuwapatia hifadhi raia wote pakizuka mapigano. Alitahadharisha juu ya hatari ya mashambulio ya kihorera. Holmes alisema taarifa alizopokea zimemthibitishia asilimia kubwa ya watu wanaouliwa Usomali ni wanawake, watoto na wale wafanyakazi wenye kuhudumia misaada ya kiutu, na alisisitiza umma huu, kwa ujumla, hauhusikani kamwe na ugomvi uliopamba nchini.

Kadhalika, katika mji wa Stockholm, Uswidin hivi sasa kunafanyika mazungumzo ya duru ya meza kuzingatia hali katika Chad. Mazungumzo haya ni ya siku mbili na lengo lake hasa ni kuwapatia wajumbe washiriki fursa ya kusailia mchango wa kuimarisha majukumu ya jumla ya Shirika la UM linalosimamia amani katika Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT). Shirika hili husaidiwa kikazi pia na vikosi vya Umoja wa Ulaya (EUFOR). Mazungumzo yaliandaliwa na Mwakilishi Maalumu wa KM katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad,Victor Angelo.

Vile vile, kuhusu Chad, ile taasisi ya Mfuko Mkuu wa UM kwa Mahitaji ya Dharura imefadhilia msaada wa dola milioni 1.2 kuhudumia vifaa vilivyounguzwa moto au kuibiwa katika mapigano yaliozuka Chad mashariki mnamo kati ya mwezi Juni. Baadhi ya posho hilo litatumiwa kuhudumia mradi wa UNHCR wa kuwapatia wahamiaji waathiriwa kutoka nje, na wale wa ndani ya nchi, vifaa vya dharura vya nyumba, kama mablangeti, mikeka, vyandarua, vitu vya jikoni, maturubali ya plastiki, mahema na pia sabuni.

KM amemteua Jane Holl Lute wa Marekani kuwa KM Mdogo Msaidizi juu ya Misaada ya Ujenzi wa Amani kwenye mataifa yanayoibuka kutoka mazingira ya uhasama na vurug.

Baraza la Usalama limekutana alasiri kupitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni za Shirika la UM la Usaidizi kwa Iraq (UNAMI) kwa miezi kumi na mbili zaidi. UNAMI vile vile imeripoti masikitiko juu ya uamuzi wa bunge la Iraq kushindwa kufikia mappatano juu ya sheria mpya za uchaguzi wa majimbo.