Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tiba ya kurefusha maisha kwa waathiriwa wa UKIMWI imepwelewa, UM kuonya

Tiba ya kurefusha maisha kwa waathiriwa wa UKIMWI imepwelewa, UM kuonya

Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa XVII juu ya UKIMWI unaendelea mjini Mexico City, Mexico. Wale viongozi wanaohusika kwenye juhudi za kueneza tiba za kurefusha maisha kwa waathiriwa wa UKIMWI kote duniani itakapofika 2010, wamearifu lengo hilo kwa sasa limepwelewa kidogo.

Kadhalika, Purnima Mane, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Muongezeko wa Idadi ya Watu (UNFPA) amebainisha "vijana wa kike 7,000 huwa wanaambukizwa virusi vya UKIMWI kila siku duniani" na ameinasihi jumuiya ya kimataifa kukithirisha mchango wao ili kukomesha hali hiyo kwa kuongeza huduma kinga dhidi ya maambukizo mapya ya virusi vya UKIMWI.

Mashirika matano yasio ya kiserekali yanayohudumia juhudi za kudhibiti uenezaji wa UKIMWI kwenye jamii zao yametunukiwa Tunzo ya Juu kabisa ya Utepe Mwekundu/Riboni Nyekundu kwenye Mkutano wa Kimataifa juu ya UKIMWI unaofanyika Mexico City. Jumuiya hizo za kiraia ziliwakilisha Ghana, Bara Hindi, Iran, Malawi na Mexico na kila mmoja ilifadhiliwa zawadi ya dola 15,000. Vile vile hapo kabla jumuiya nyengine za kiraia 25 zilizotambuliwa mchango wao katika kupiga vita UKIMWI kila mmoja ilitunzwa zawadi ya dola 5,000. Washindi hawa ni miongoni mwa mashirika yasio ya kiserekali 550 kutoka nchi 147 ambayo yalizingatiwa kwenye mashindano yanayoungwa mkono na UM kutambua jamii zinazoshiriki katika kunusurisha umma na hatari ya janga maututi la UKIMWI.