Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wabainisha wahka juu ya maamuzi ya Mahakama ya Kukabili Ugaidi Sudan

UM wabainisha wahka juu ya maamuzi ya Mahakama ya Kukabili Ugaidi Sudan

Mwakilishi Maalumu wa KM kwa Sudan, Ashraf Qazi, Alkhamisi alitoa taarifa rasmi iliotathminia hukumu ya kifo iliopitishwa karibuni na Mahakama ya Kukabili Ugaidi ya Sudan, dhidi ya wafuasi 30 wa kundi la waasi la JEM, taarifa ambayo ilibainisha wasiwasi wa UM juu ya uamuzi ambao ilisema haulingani na viwango vya sheria ya kimataifa.

UNMIS iliripoti vile vile kwamba utaratibu wa kimahakama chini ya Sheria Dhidi ya Ugaidi hauwawezeshi watuhumiwa kuwa na fursa inayoridhisha ya kukata rufaa ya kupinga madai ya hukumu. UNMIS imesema inatambua kihakika kwamba Serikali ya Sudan ina haki na uhalali wa kushtaki na kuhukumu wale watu walioshiriki kwenye makosa ya jinai yanayoambatana na shambulio la mji wa Omdurman, lakini pia inakumbusha ya kuwa Serikali inaposimamia kesi hiyo inatakiwa ihakikishe inaendesha mashitaka kwa hatua za kisheria zinazolingana na viwango vya sheria ya kimataifa. Halkadhalika UNMIS imeihimiza Sudan kujitahidi kuondosha hukumu ya kifo kwa sasa hivi, kama ilivyopendekezwa na Baraza Kuu la UM mwezi Novemba mwaka jana (2007).