Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti wiki iliopita lilifanikiwa kuendeleza operseheni ya kuwachanja watoto, karibu milioni mbili, chini ya umri wa miaka mitano, nchini Zimbabwe.

UNICEF ilifanikiwa kuhudumia afya watoto wote hawa, hata wale watoto wanaoishi kwenye maeneo yaliopo mbali na ambayo yana shida kuyafikia, wote walibahatika kupatiwa chanjo kinga dhidi ya maradhi mbalimbali yanayosumbua watoto wachanga, mathalan chanjo dhidi ya kifua kikuu, shurua, dondakoo, peopopunda, kifaduro, homa ya manjano, homa ya mafua na pia maradhi ya kupooza. Licha ya kuwa UNICEF inaendeleza kazi zake Zimbabwe kama kawaida haiwezi kukamilisha miradi ya kuhudumia watoto kama inavyotakikana kwa sababu ya upungufu wa mchango wa yale mashirika yasio ya kiserekali, ambayo yalipigwa marufuku na Serikali ya Zimbabwe kutumikia jamii hizo tangu Juni 04 (08).

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti Djibouti sasa hivi inakabiliwa na mzozo wa kiutu unaosukumwa na mchanganyiko wa matatizo kadha, yanayojumuisha kuwepo ukame wa miaka mingi, uhaba wa mvua, na muongezeko mkubwa wa bei za chakula na mafuta katika soko la kimataifa. Hali hiyo vile vile inaghumiwa na mmiminiko katika Djibouti wa wahamiaji Wasomali waliohajiri makwao kunusuru maisha. Serikali ya Djibouti pamoja na UM wameanzisha kampeni maalumu yenye mwito wa kutaka ifadhiliwe, na wahisani wa kimataifa, dola milioni 32 zitakazotumiwa kukidhi mahitaji ya kihali nchini humo katika miezi sita ijayo.