Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

BU lashughulishwa na mzozo wa Ossetia ya Kusini

BU lashughulishwa na mzozo wa Ossetia ya Kusini

Baraza la Usalama bado linaendelea kushughulishwa na mzozo wa Ossetia ya Kusini, jimbo liliojitenga la Georgia ambapo mapigano yameshadidia kwa kasi huko tangu wiki iliopita. Baraza limekutana kwa mara ya tano hii leo kushauriana, kuhusu taratibu za kuchukuliwa kipamoja kuwasilisha suluhu ya kuridhisha, baada ya kuzuka mapigano makali baina ya vikosi vya Urusi na Georgia kwenye eneo hilo. katika mashauriano hayo wajumbe wa Baraza wameshindwa tena kukubaliana maamuzi ya kuridhisha kusitisha mapigano na kuruidisha utulivu na amani ya eneo.

Baraza la Usalama lilikutana tena Ijumapili na baada ya kikao kumalizika, bila kufikia suluhu, Balozi Jan Grauls wa Ubelgiji, Raisi wa Baraza kwa mwezi Agosti aliwaambia waandishi habari Makao Makuu kwamba wajumbe wa Baraza la Usalama wamedhaminiwa jukumu adhimu kimataifa la kuhakikisha usalama na amani unarejea haraka katika eneo la uhasama Ossetia Kusini. Alisema kwa mujubu wa taarifa alizozisikia kwenye mahojiano ya Baraza asubuhi Ijumapili, Marekani na Ufaransa wameamua kutayarisha azimio litakalowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama kubainisha hatua za kuchukuliwa na Baraza kuelezea hali ilivyo katika Ossetia Kusini.

Edmond Mulet, Msaidizi KM katika Idara ya Operseheni za Ulinzi Amani za UM (DPKO) aliripoti kwenye kikao cha faragha, mbele ya Baraza la Usalama, kwamba mzozo maututi umeshasambaa sasa hivi nje ya mipaka iliokiuka jimbo la uhasama la Ossetia Kusini. Kadhalika, alisema vikosi vya uangalizi vya UM vya UNOMIG vilivyokuwepo kieneo tangu 1993, kuchunguza kusimamishwa kwa mapigano baina ya Georgia na wenye madaraka kwenye jimbo la Abkhazia, Georgia kaskazini-magharibi, viliarifiwa viondoshe askari wao kutoka Bonde la Kodori ya Juu kwa sababu ya ukosefu wa usalama, na inakhofiwa mapigano mapya huenda yakzuka huko, hali kadhalika.

Antonio Guterres, Kamishana Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ameripotiwa akisema ameridhika na uamuzi wa Urusi na Georgia kuruhusu kutumiwa njia maalumu za amani na zilizo salama, kuhudumia misaada ya kiutu kwa kuwahamishia wale raia waliongo’lewa makazi kwa sababu ya mapigano katika Ossetia Kusini. UNHCR inaandaa kupeleka ndege ya shehena za misaada ya kiutu kutokea Dubai leo usiku leo kuelekea Georgia, ndegeambazo zitabeba mablangeti 20,000 pamoja na vifaa vyengine vinavyohitajika kukidhi mahitaji ya dharura ya umma waathiriwa kwenye jimbo la Caucasus, na pia kupeleka wafanyakazi ziada wanaohudumia misaada ya kiutu.

Halkadhalika, Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) nalo vile vile limeanzisha opersheni maalumu za kugawa misaada ya chakula kukidhi mahitaji ya siku 10 ya watu 2,000 ziada waliong’olewa makazi abao sasa wanaishi kwenye mastakimu ya muda katika Tbilis, mji mkuu wa Georgia, kwa kutika ombi la Serikali ya Georgia.