Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM ameripoti kuchukizwa hadi na ripoti aliyopokea kuhusu matokeo ya upelelezi wa Ofisi ya UM Kuchunguza Makosa ya Huduma za Ndani, ambayo ilifichua ushahidi unaojitosheleza kuhusu vitendo vya makansdamizo ya kijinsia yalioendelezwa siku za nyuma na moja ya vikosi vya Bara Hindi vilivyoambatishwa na Majeshi ya Ulinzi wa Amani ya UM katika JKK (MONUC).

Vikosi hivyo vilituhumiwa kushiriki kwenye udhalilishaji wa kijinsia na kuvunja sheria dhidi ya haki za wanawake. Kwenye risala yake KM alisisitiza, kwa kauli ilio nzito kabisa, kwamba ifahamike wazi kabisa makosa hayo ni karaha isiyokubalika, wala kustahamilika kamwe, na pindi yakithibitishwa Serikali ya India itawajibika kuchukua hatua kali kabisa, kwa kutoa adhabu ya kima cha juu, kufundisha nidhamu dhidi ya wale wanajeshi wote waliohusika na jinai hiyo, kwa kufuatana na sheria ya nchi.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afrika Magharibi, Said Djinnit amerejea Dakar, Senegal wiki hii yalipo ofisi zao baada ya kuzuru Mauritania kwa siku tatu ambapo alipata fursa ya kukutana, kwa mazungumzo, na viongozi wa baraza la majeshi yaliopindua serikali. Kwenye mazungumzo hayo Djinnit aliwahimiza viongozi hao kurejesha haraka uatawala wa kikatiba nchini. Kadhalika, alimbainishia kiongozi wa baraza la majeshi, Jenerali Abdelaziz, ambaye sasa anaongoza Baraza Kuu la Taifa, masikitiko kuwa seikali halali imepinduliwa mnamo tarehe 06 Agosti, na alikumbusha kitendo hicho kimelaaniwa, kwa kauli moja, na jumuiya nzima ya kimataifa.

Shirika la Muungano wa Posta Ulimwenguni (UPU) liliokutana kwa wiki tatu kwenye kikao cha ishirini na nne cha Mkutano Mkuu wa Posta za Ulimwengu kimekamilisha mijadala yake Ijumanne ya leo mjini Geneva. Miongoni mwa maamuzi yaliochukuliwa kabla ya kikao kufungwa ni pamoja na uchaguzi wa Edouard Dayan wa Ufaransa, ambaye alitakiwa aendelee kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya UPU, na Guozhing Huang wa Uchina aliteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na wanatarajiwa kusimamia madaraka kwa kipindi cha kuanzia 2009 mapaka 2012. Kenya imeteuliwa kuchukua nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Utawala, na Ugiriki imechaguliwa kuwa Kiongozi wa Baraza la Operesheni za Posta. Mkutano Mkuu wa Posta za Uliwengu mwengine utafanyika tena katika 2012 kwenye mji wa Doha, Qatar.