Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Wajumbe wa kamati mbili za kufuatilia utekelezaji wa Maafikiano ya Djibouti kuhusu Amani Usomali wametangaza kwamba watakutana mwisho wa wiki katika Djibouti, kwa mara nyengine tena, kuzingatia masuala ya kurudisha utulivu na amani nchini.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya mashauriano na wawakilishi wa Serikali ya Mpito ya Shirikisho la Usomali na pia wawakilishi wapinzani wa Ushirikiano wa Makundi ya Ukombozi wa Pili wa Usomali. Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah, ameyakaribisha maendeleo haya na kuiomba jamii ya kimataifa kuunga mkono kikamilifu juhudi za amani katika Usomali, na kuchangisha msaada wao kwa umma wa taifa hilo ili uweze kusuluhisha masaibu waliokabiliwa nayo kwa utaratibu wa kuridhisha.

Francois Lonseny Fall, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, ametangaza kuwa na wasiwasi mkuu juu ya hali ya usalama katika eneo la kaskazini-mashariki ya nchi. Ameshutumu tukio la mashambulio ya kutumia risasi yaliozuka tarehe 07 Agosti baina ya vikosi vya serikali na kundi la waasi la APRD. Fall alionya tukio kama hilo linahatarisha mapatano ya kuacha mapigano na maafikiano ya amani yaliotiwa sahihi na makundi yanayohasimiana mwezi Mei mwaka huu. Kwa hivyo, Fall aliyataka makundi yote mawili husika kuonyesha ustahamilivu mkubwa na kutekeleza maafikiano yao kama ilivyoidhinishwa kabla. Kadhalika Fall alihimiza sheria ya kutoa msamaha iidhinishwe haraka na wenye madaraka, kitendo ambacho anaamini kikitekelezwa kitasaidia kuanzisha utaratibu wa kupokonya silaha makundi ya kisiasa na, hatimaye, kuwakusanya wafuasi hao kwenye kambi za wanajeshi na kuwajumuisha na jeshi la taifa.