Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya wahudumia misaada ya maendeleo Afghanistan yanalaaniwa na Mkuu wa UNAMA

Mauaji ya wahudumia misaada ya maendeleo Afghanistan yanalaaniwa na Mkuu wa UNAMA

Kai Eide, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan ambaye pia anaongoza Shirika la Usaidizi la UM Afghanistan (UNAMA) ameripoti kuchukizwa sana na taarifa aliopokea juu ya vifo vya wafanyakazi watatu wanawake, waliohudumia misaada ya kiutu pamoja dereva wao, raia wa Afghanistan, ambao waliuawa baada ya gari lao kushambuliwa leo asubuhi na watu wasiojulikana, waliokuwa wamechukua silaha, wakati wakielekea Logar kutokea Kabul.

Aliihimiza Serikali ya Afghanistan, kujitahidi kama inavyoweza, kuhakikisha waliofanya makosa hayo wanashikwa na kufikishwa mahakamani. Alitahadharisha kwamba hivi sasa Afghanistan imekabwa na vizingiti vikubwa aina kwa aina dhidi ya utu, na aliyataka makundi husika yote kutambua kwamba misaada ya kiutu inayopelekewa Afghanistan haina upendeleo, na hufadhiliwa kuhudumia idadi kubwa ya raia walio dhaifu wanaohitajia misaada ya kihali itakayowawezesha kuishi kikawaida.