Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathiriwa wa mapigano Georgia kupatiwa msaada wa chakula na WFP

Waathiriwa wa mapigano Georgia kupatiwa msaada wa chakula na WFP

Ndege mbili za aina ya Antonov 12 zilizokodiwa na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) leo asubuhi zilianza safari ya kuelekea Georgia kutokea mji wa Brandisi, Utaliana zikibeba shehena ya tani za metriki 34 za biskuti maalumu za chakula zitakazogaiwa maelfu ya watu waliongo’lewa makwao ambao walidhurika kihali na mapigano yalioshtadi karibuni kwenye eneo lao.

KM ameripotiwa kuyakaribisha makubaliano ya Georgia na Shirikisho la Urusi kuridhia utaratibu wa kurudisha amani uliotayarishwa, na kupendekezwa, na Raisi wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy. KM alihimiza mpango huo wa amani utekelezwe, halan, kwa kuambatana na kanuni za mwafaka, ikijumuisha ile rai ya kukomesha hali yote ya uadui kati yao, na kuwataka wahamishe vikosi vyao kutoka maeneo ya mapigano na kuvirudisha kwenye zile sehemu ambazo majeshi yao yaliegesha katika siku za nyuma kabla ya mapigano.