Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ofisi ya UM Geneva imeripoti Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) anatazamiwa kuelekea Georgia na Shirikisho la Urusi wiki ijayo kufanya tathmini ya operesheni za kuhudumia misaada ya kiutu kwenye sehemu zilizoathirika na mapigano ya karibuni. Kadhalika, Guterres atakutana kwa ushauriano na serikali za mataifa mawili hayo juu ya mahitaji yanayotakiwa kutoka mashirika ya kimataifa ili kukidhi haja za waathiriwa wa vurugu la eneo lao.~

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti watumishi wa mashirika ya kuhudumia misaada ya kiutu ya UM wamejiandaa kwenye ardhi za Georgia na Shirikisho la Urusi kwa sasa wakisubiri idhini itakayowawezesha kuendeleza shughuli zao kwa usalama. Ijumatatu, tarehe 18 Agosti (08) mashirika ya UM yataanzisha kampeni ya kuomba yafadhiliwe mchango wa kimataifa kuhudumia misaada ya kiutu katika Georgia na Urusi. Hivi sasa OCHA imeshasajilia kupokea mchango wa dola milioni 14.8 na kuahidiwa pia mchango ziada wa dola milioni 1.5 kutoka wahisani wa kimataifa.

Kamati ya Msalaba mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) imeripoti kwamba wenye madaraka, kimsingi, wameidhinisha kupeleka wafanyakazi wao katika eneo la Ossetia Kusini, bila vizuizi. Lakini watuimishi wa ICRC, juu ya kuwa wameshajiandaa kuelekea huko, hawatoelekea kwenye eneo la vurugu mpaka watakapohakikishiwa usalama wao.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) lina wasiwasi kuhusu usalama wa wahudumia misaada ya kiutu katika Ossetia Kusini. UNICEF inakhofia mgogoro wa eneo hilo kama haujadhibitiwa mapema huenda ukasota na kuendelea hadi wakati wa majira ya baridi na ukaathiri sana afya ya watoto. UNICEF kwa sasa inapeleka kwa ndege misaada ya kuhudumia maji safi na salama, vifaa vya dharura kwa maskuli na zana za kupumzikia kwa watoto na wahamiaji wa ndani waliojikuta kwenye maeneo yaliokosa vifaa hivyo.

Mshauri Maalumu wa KM kwa Myanmar, Ibrahim Gambari ataondoka New York Ijumaa kwa ziara ya siku tano katika Myanmar kuanzia Ijumatatu, Agosti 18 baada ya mwaliko wa Serikali ya Myanmar kwa mashauriano.

Timu ya uchunguzi ya pamoja ya UM na Jumuiya ya Maendeleo ya Ucghumi kwa Afrika Magharibi (ECOWAS) imebuniwa leo Abuja, kuongoza upelelezi kuhusu vifo vya raia kadha wa Ghana waliokutikana wamezikwa katika taifa la Gambia katika 2005.

Kamati ya Ushauri ya Baraza la UM juu ya Haki za Binadamu imekamilkisha mjini Geneva kikao chake cha awali ambapo ilipitisha, kwa kauli moja, maazimio kumi na tatu kuzingatiwa na Baraza, ikijumuisha haki ya chakula kwa wale walioathiriwa na mgogoro wa mifumko ya bei za chakula kwenye soko la kimataifa, na vile vile masuala yanayofungamana na haki ya ilimu.