Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za utatuzi wa mzozo wa Ossetia Kusini zaendelea UM

Juhudi za utatuzi wa mzozo wa Ossetia Kusini zaendelea UM

Ijumanne alasiri Baraza la Usalama lilikutana kwa mara ya sita kuzingatia tena hali katika Georgia na mgogoro wa Ossetia Kusini, na wajumbe wa Baraza walishindwa kufikia suluhu ya kuridhisha. ~

Mashirika ya UM ya UNHCR na WFP, kwa mara ya kwanza tangu mzozo kuanza katika Ossetia Kusini wiki mbili nyuma, yamefanikiwa kuanzisha huduma za kugawa misaada ya kiutu kwa maelfu ya waathiriwa wa mapigano kwenye sehemu za Georgia magharibi. WFP ilipeleka misaada ya chakula katika vijiji vya wilaya ya Kaspi na mji wa Senaki - Georgia magharibi - lakini ugawaji huo ulisitishwa kwenye wilaya ya Alkhalgori – jirani na Ossetia Kusini – kwa sababu ya hali isiyotarajiwa ilijiri ambapo wakazi wa eneo walihajiri makwao kujiepusha na mapigano. Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) nayo imeripoti kushuhudia maendeleo katika siku za karibuni kwenye huduma za kiutu, baada ya wenye madaraka kuruhusu misafara ya misaada hiyo inayopelekwa eneo liliokuwa na vurugu kuvuka, kwa usalama, vile vizuizi viliowekwa vya barabarani, licha ya kuwa fursa ya kuvuka baina ya maeneo ya mashariki na magharibi bado ni ndogo. Lakini hata hivyo, OCHA ilisema, mashirika ya kimatafa yanayohudumia misaada ya kiutu sasa yanaweza kwenda kwenye maeneo yaliokuwa na matatizo kuyafikia katika siku za nyuma, ikijumlisha barabara inayoelekea bandari ya Poti.

Kadhalika kuhusu Georgia tumearifiwa, kwa mara ya awali tangu mgogoro wa Ossetia Kusini kuzuka, wafanyakazi wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (ICRC) wameruhusiwa leo hii kuingia kwenye jimbo hilo la Georgia kuhudumia umma muathiriwa. Raisi wa ICRC, Jakob Kellenberger, ambaye amerejea karibuni kutoka ziara ya siku tatu katika Georgia na Urusi, alithibitisha kwenye mazungumzo na waandishi habari ya kuwa Urusi inaunga mkono rai ya kupeleka huduma za kiutu kwenye eneo la mgogoro, hasa kwenye mji mkuu wa Ossetia Kusini wa Tskhinvali, kutathminia mahitaji na kusaidia umma ulioathirika na mapigano ya karibuni. Kellenberger kwenye mahojiano na Redio ya UM-Geneva alielezea aina ya misaada timu ya ICRC imeandaa kwa Ossetia Kusini kwa hivi sasa:

"Katika timu yetu, tuna madaktari wapasuaji, tuna watalamu wanaohusika na hifadhi za raia panapozuka uhasama, na vile vile wataalamu wa kudhibiti usalama wa kiuchumi. Lengo la ujumbe huu ni kuanzisha mawasiliano tena na wenye madaraka ili kutathminia kihakika hali halisi ilivyo kieneo, hususan kuambatana na mahitaji ya ulinzi wa raia na pia huduma zinazotakikana kidharura kusaidia kihali umma waathiriwa.”