Hapa na pale
KM amelaani mashambulio mawili ya mabomu ya kujitolea mhanga yaliofanyika Alkhamisi katika mji wa Wah, Pakistan, tukio ambalo lilisababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi wingi wa kiraia. Alirudia msimamo wake juu ya vitendo vya kigaidi, vya kihorera, ambavyo alisisitiza ni vya kulaumiwa na na anavipinga kihakika. KM alituma mkono wa huzuni kwa aila ya waathiriwa, Serikali na umma wa Pakistan.
Kemal Dervis, Msimamizi wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) ametoa taarifa maalumu inayosailia Duru ya Mazungumzo ya Doha. Taarifa ya Dervis ilisema mazingira ya uchumi katika soko la kimataifa umo kwenye mkondo unaohitajia mfumo wa biashara wenye wahusika wingi, na ulio wa haki, na wenye usawa na uwazi, hasa tukizingatia hali ya kuregarega kwa uchumi wa dunia kwa sasa hivi inashtusha na matatizo yanayobashiriwa na wataalamu kujiri katika siku zijazo yanahitaji kudhibitiwa mapema. Alisema anaunga mkono, kidhati, pendekezo la Raisi wa Benki Kuu ya Dunia, Robert B. Zoellick pamoja na Pascal Lamy, Mkurugenzi-Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) la kuhimiza mazungumzo ya Duru ya Doha yarudiwe tena haraka. Alisisitiza maafikiano ya Doha yangelikamilishwa kama ilivyotarajiwa, yangeliwasilisha natija kubwa za uchumi katika nchi zinazoendelea na kwenye uchumi wa dunia. Alisema anaamini suluhu inaweza kupatikana mataifa yakiweza kuondosha vile vizingiti vilivyosalia, vinavyokwamisha mapatano ya mwisho, hususan ule mpango wa kutoa ruzuku kinga kwa wakulima wa mataifa yenye maendeleo ya viwanda.