Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polisi wa JKK wapatiwa na MONUC mafunzo ya kudhibiti udhalilishaji wa kijinsiya

Polisi wa JKK wapatiwa na MONUC mafunzo ya kudhibiti udhalilishaji wa kijinsiya

Shirika la UM Linalosimamia Huduma za Ulinzi wa Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) limeripoti kwamba limefanikiwa kukamilisha mafunzo maalumu kwa maofisa wa polisi, juu ya taratibu za kisheria za kutumiwa nao katika kudhibiti makosa ya jinai ya kijinsiya yanaambatana na fujo na matumizi ya nguvu na mabavu dhidi ya wanawake.

Ilivyokuwa matatizo ya kijinsiya yanayohusu utumiaji mabavu na nguvu dhidi ya wanawake yameonekana kutanda kwa wingi katika JKK, mashirika yasio ya kiserikali ya kitaifa, na kimataifa, yaliamua kujiunga na Serikali kwenye juhudi za kukabiliana kipamoja na janga hili na, mwishowe, kulikomesha. UM, kwa upande wake, ulidhaminiwa madaraka ya kusimamia masuala yanayohusu sheria na mahakama na ulitakiwa uwasaidie waathiriwa wa unyonyaji/unyanyasaji wa kijinsiya kutekelezewa haki zao halali za kimsingi kwa kulingana na sheria.

Mnamo mwezi huu wa Agosti maofisa wa polisi 37, wakijumlisha mainspekta na wapelelezi kutoka sehemu za Beni, Butembo na Lubero - katika jimbo la Kivu Kaskazini – walibahatika kupatiwa kuhudhuria masomo maalumu nchini kuhusu taratibu mpya za kutumiwa na maofisa wa kimahakama, na katika kuimarisha majukumu yao ya kikazi, kwa kulingana na sheria. Mara nyingi maofisa wa usalama katika JKK hudhaminiwa madaraka ya kufanya upelelezi kuhusu makosa ya jinai ya kijinsiya, ambapo waathiriwa na mashahidi husika hutishwa na kuhitajia ulinzi na hifadhi inayoaminika kutoka mapolisi. Mafunzo ya MONUC yatasaidia kuyatekeleza hayo. Vile vile washiriki wa mafunzo ya MONUC walielimishwa nidhamu za kutumiwa kutafisiri sheria za kitaifa, na kimataifa, zinazoambatana na jinai ya kijinsiya ya kutumia mabavu. Maofisa hawa wanatarajiwa kurejea kwenye maeneo yao kusaidia kudhibiti bora waathiriwa wa maafa ya udhalilishaji wa kijinsiya.

Hali kadhalika, MONUC imefanikiwa kuzipatia darzeni za batalioni za jeshi la taifa la JKK la FARDC masomo maalumu juu ya hifadhi kinga za watoto, na kuhusu haki za binadamu; na vile vile walipatiwa mafunzo yanayohusu udhibiti bora wa jinai ya udhalilishaji wa kijinsiya na sheria ziada za kutunza haki za kijeshi. Hivi sasa MONUC inaendelea kuisaidia Serikali ya JKK (DRC) kuunda vikosi vitakavyojaaliwa ubingwa wa kitaaluma, na inatarajia itakapofika Septemba 2009 kukamilisha mafunzo kuhusu haki za binadamu kwa batalioni 28 za jeshi la taifa la FARDC.