Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ameerah Haq, Mshauri Mkazi juu ya Huduma za Kiutu za UM kwa Sudan amesema Umoja wa Mataifa una khofu kuu kuhusu ripoti ilizopokea Ijumatatu asubuhi zenye kuonyesha magari ya polisi wa Sudan yaliizingia kambi ya Kalma, iliopo kilomita 25 kutoka mji wa Nyala, Darfur Kusini ambapo wahamiaji wa ndani (IDPs) wamepatiwa makazi ya muda. Taarifa ziliofuatia zilisema kambi ya Kalma ilishambuliwa baadaye na kusababisha vifo vya raia na majeruhi kadhaa.

Kadhalika, taarifa ya Haq ilisema vitendo hivyo viliashiriwa kuhatarisha usalama wa raia ambao, kwa mujibu wa Sheria ya Kiutu ya Kimataifa, wanawajibika kupatiwa hifadhi na ulinzi wa kuridhisha na wenye madaraka panapofumka mazingira ya uhasama. UM imetoa mwito unaohimiza kuwepo uvumilivu, na kupendekeza kuanzishwe haraka ushoroba wa kiutu utakaotumiwa kuwahamishia raia majeruhi kutoka kwenye eneo la uhasama na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo watapatiwa matibabu.

Wahamiaji wa ndani ya nchi 80,000 wingi wao wao wakiwa watoto na wanawake wamesajiliwa kuishi kwenye Kambi ya Kalma.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould-Abdallah amenakiliwa akisema kuwa na masikitiko makubwa juu ya mauaji ya kihorera ya raia wasio hatia, yaliotukia kwenye mji wa Kismayo karibuni na kusababisha mamia elfu ya wakazi kuhajiri makwao. Ould-Abdallah alisema anaamini udhibiti wa bandari ya Kismayo na mapato yanayokusanywa hapo yalikuwa ndio chanzo kinachochochea uhasama. Alisema anasikitishwa sana na mapigano ya kutumia bunduki kwenye miji ya Afgooye na Mogadishu ambapo idadi kubwa ya watu waliuawa, na raia kadha walijeruhiwa na kusababisha watu 2,000 kung’olewa makwao. Mjumbe wa KM alitoa mwito wenye kuyataka makundi yote yanayohasimiana Usomali kuhishimu haki za kimataifa za kibinadamu na vile vile haki za kiutu, na wajibu wao wa kuyatekeleza mapatano ya amani ya Djibouti kidharura ili kuepusha raia na janga la mapigano.

KM Ban Ki-moon ameipongeza Serikali pamoja na umma wa Uchina kwa juhudi zao zisio mfano, za kukirimu na kusimamia Mashindano ya Olimpiki ya kihistoria kabisa yaliofanyika mjini Beijing katika wiki mbili zilizopita. Alisema Mashindano haya ya Kiangazi 2008 yaliupatia umma wa kimataifa fursa muhimu ya kuendeleza amani kwa walimwengu na kuwasilisha utulivu kwa kutilia mkazo watu kufahamiana, kukirimiana na kushirikiana kwa ari ya kiOlimpiki ya kutumikia umma.