Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Taarifa kwa waandishi habari iliotolewa Ijumanne (26/08/2008) na Shirika la Mchanganyiko la UM/UA Kulinda Amani Darfur (UNAMID) kuhusu mashambulio ya kambi ya wahamiaji wa ndani (IDPs) ya Kalma, iliopo katika jimbo la magharibi la Sudan, ilishtumu, kwa lugha ya uzito mkuu, kitendo cha kutumia mabavu ya kuua yaliokiuka mipaka na yasiowiana kilichoendelezwa na vikosi vya usalama vya Serikali ya Sudan dhidi ya raia, kitendo ambacho UNAMID ilisisitiza kilitengua haki za kimsingi na kusababisha ajali mbaya ya vifo na majeruhi kwa wakazi katika kambi hiyo.

UNAMID imesisitiza kwamba hali ya kuwepo kwa silaha kwenye kambi za wahamiaji hubatilisha hadhi ya kambi za IDP katika sheria ya kiutu ya kimataifa, ya kupatiwa hifadhi ya kutodhuriwa. Jamii ya IDP, viongozi na wawakilishi wao wote walinasihiwa kuhakikisha kambi zao zinasalia kuwa maeneo yalio huru na silaha za aina yoyote.

Licha ya kuwa madai ya kuwepo kwa silaha ndani ya kambi ya Kalma ni suala la kutaharakisha wenye madaraka Sudan juu ya usalama, hata hivyo hatua zilizochukuliwa kukabiliana na mvutano uliojiri kwenye kambi ya Kalma zinaharamisha mutlaki yale Mapatano ya Amani ya Darfur.

Kesi ya Ephrem Setako, aliyekuwa Liuteni Kanali katika jeshi la Rwanda imeanza rasmi Ijumanne (26/08/2008) mjini Arusha mbele ya Mahakama ya UM juu ya Rwanda. Setako anakabili mashitaka sita kuhusu mauaji ya halaiki, na kushiriki katika njama ya mauaji ya maangamizi, jinai dhidi ya utu na makosa kadha ziada yalioharamisha Mikataba ya Geneva juu ya udhibiti wa ukatili katika vita. Setako aliposhikwa Uholanzi mnamo Novemba 2004 alikana makosa yote hayo. Wakili mtetezi Lennox Hinds alikataa kuwakilisha kauli ya ufunguzi wa utetezi kwa hivi sasa.

Ofisi ya UM dhidi ya Uhalifu na Madawa ya Kulevya (UNODC) imewasilisha Ripoti ya Uchunguzi wa Kasumba katika Afghanistan kwa 2008 inayosema ukulima wa afyuni nchini humo uliteremka kwa asilimia 19 kwa mwaka huu. Mukhtasari wa ripoti ulionyesha hali bado ni “dhaifu na huenda ikazuka tena” kwa kasi pindi jumuiya ya kimataifa itashindwa kuyapatia malipo mazuri majimbo hayo. Kwa mujibu wa ripoti uzalishaji wa kasumba kwa mwaka huu ulifanyika kwenye eneo la hekta 157,000 - kiwango ambacho ni cha chini kidogo tukilinganisha na mavuno ya hekta 193,000 katika 2007. Takwimu hii humaanisha idadi ya majimbo yaliojikomboa na zao la kasumba katika Afghanistan imeongezeka kwa karibu asilimia 50%: kutoka majimbo 13 na sasa kuwa majimbo 18, hali matokeo ambayo yanaashiria kasumba haipandishwi tena katika zaidi ya nusu ya majimbo 34 yaliopo katika Afghhansitan.