Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Aliyekuwa msemaji wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Yugoslavia ya Zamani (ICTY), Florence Hartmann ameshitakiwa kuiaibisha Mahakama na kudharau madaraka yake kwa madai ya kwamba alifichua, mara mbili, taarifa za siri zinazohusu kesi ya aliyekuwa Raisi wa Serbia, Slobodan Milošović. Hartmann ameamrishwa kuhudhuria Mahakama ya ICTY mjini Hague, Uholanzi Septemba 15, 2008 kusikiliza mashitaka.~

Mazungumzo ya wiki moja yalioongozwa na UM kusailia masuala muhimu kuhusu mkataba mpya wa kudhibiti kipamoja athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani, yaliofanyika Accra, Ghana yamekamilishwa kwa maafikiano ya kutia moyo, kwa mujibu wa taarifa ya Yvo de Boer, Mkurugenzi Mkuu wa Mkataba wa UM juu ya Mfumo wa Kuzingatia Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC). Mkutano wa Accra ni miongoni mwa mifululizo ya vikao vilivyodhaminiwa na UM vinavyoitishwa kuandaa maafikiano ya kuwasilisha mkataba mpya, baada ya Mkataba wa Kyoto kumaliza madaraka yake katika 2012 kuhusu kima cha udhibiti wa hewa chafu inayomwagwa angani na mataifa yalioridhia mkataba. De Boer alisema “jambo muhimu liliopatikana” kwenye kikao cha Accra ni mwafaka wa kumpa Mwenyekiti wa kundi la utendaji ushirikiano wa muda mrefu katika ukusanyaji wa mapendekezo yote yaliofikiwa na nchi wanachama hadi sasa, pamoja na mapendekezo yatakayofuatia katika wiki zijazo. Kwa hivyo, aliongeza kusema de Boer, mafanikio haya ya Accra yatayasaidia Mataifa Wanachama kuwa na “msingi halisi wa kuanzisha majadiliano yenye uzito mkubwa” kuhusu taratibu za kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani, hususan katika kikao kijacho kitachofanyika Poznan, Poland kuanzia tarehe 01 hadi 12 Disemba 2008.