Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Naibu KM wa UM, Asha-Rose Migiro pamoja na maofisa wenzi wanaohusika na maandalizi ya ratiba ya kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) kwa Afrika, wamewasilisha ripoti yao mnamo siku ya mwisho ya Mkutano wa Umoja wa Afrika unaofanyika Sharm el-Sheikh, Misri.

Ripoti imeorodhisha mapendekezo yanayolenga kwenye zile juhudi za kuwasilisha mapinduzi ya kilimo barani Afrika, na hatua za kuchukuliwa kuimarisha sekta za afya ya jamii na elimu, na pia miradi inayohitajika kuziba pengo muhimu linalohusu miundombinu ilio khafifu na mitandao ya biashara. Ripoti vile vile imetaka kuona Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA) inatolewa kwa utaratibu unaotabirika na kuongeza mitaji yenye thamani.

Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba kuanzia Julai mosi 2008, bei za vitabu vyote vinavyochapishwa na mashirika yake, itapunguzwa kwa asilimia 75 kwa zile nchi zilizo masikini sana, na kwa asilimia 50 kwa mataifa yanayoendelea. Uamuzi huu utawasaidia wanafunzi, walimu, wasomi watafiti pamoja na taasisi ziliopo katika nchi masikini kuwa na uwezo wa kununua, kwa bei nafuu, vitabu na majarida ya UM yanayozingatia masuala yanayohusu ulinzi wa usalama na amani, haki za wanawake, hifadhi ya mazingira, huduma za maendeleo ya miji na afya ya jamii, haki za binadamu, sheria za kimataifa na udhibiti wa uhalifu unaovuka mipaka, uongozaji wa biashara kwenye soko la kimataifa, maendeleo ya teknolojiya pamoja na masuala mengineyo yanayopewa umuhimu na umma wa kimataifa. Mataifa mengi yanayoendelea hayamudu gharama za kununua vitabu vinavyochapishwa na UM; matahalan, Kitab cha Matukio ya Mwaka cha UM kinagharamiwa $175, lakini kutokana na utaratibu mpya wa UM utagharamia nchi masikini hivi sasa nusu au robo ya bei hiyo, kwa kulingana na uwezo wao wa uchumi kijumla.

Tarehe 01 Julai huadhimisha miaka arobaini ya tangu Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Kinyuklia (NPT) uliporuhusiwa kutiwa sahihi ya kuridhia na Mataifa Wanachama. Licha ya kuwa Mkataba wa NPT unakabiliwa na vizingiti aina kwa aina, mafanikio kadha, ya kiawamu, yalipatikana katika kipindi hicho. KM alisema kazi kubwa bado imesalia inayohitajia mchango wa umma wa kimataifa kwenye bidii za kuhakikisha ulimwengu unakuwa huru na janga la silaha za kinyuklia.