G-8 inatakiwa izingatie kihakika mifumko ya bei za chakula na mafuta duniani
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwenye ripoti mpya iliotolewa wiki hii, imekumbusha kwamba mfumko wa bei za chakula pamoja na muongezeko wa kasi wa bei za mafuta katika soko za kimataifa, ni vitendo vinavyoathiri sana nchi masikini na yale mataifa ya maendeleo ya wastani, nchi ambazo kikawaida hulazimika kuagizishia bidhaa hizo kutoka nje.
Raisi wa Benki Kuu ya Dunia Robert Zoellick amemtumia Waziri Mkuu wa Ujapani Yasua Fukudo pamoja na KM wa UM na viongozi wengine wa Kundi la G-8 barua yenye kuonya kwamba kupanda kwa bei za chakula na mafuta ulimwenguni ni tatizo linalosababisha ugawaji mkubwa wa mapato, usiokuwa sawa, hali ambayo hupalilia ufukara na kuzusha ugeugeu wa kijamii; na alisema ilivyokuwa “maafa haya yamesababishwa na wanadamu na sio maumbile” inawajibika kwa wanadamu pia kuandaa miradi inayofaa ya kurekibisha hali hiyo, itakayoleta natija za umma. Aliyahimiza mataifa ya Kundi la G-8 na zile nchi kuu zinazolisha mafuta, kulenga suluhu zao katika kuchangia misaada ya dharura, itakayotumiwa, haraka iwezekanavyo, kukidhi mahitaji ya mataifa dhaifu kiuchumi, hasa katika shughuli za kukuza kilimo, na kufadhilia Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) na Benki Kuu ya Dunia fedha zinazohitajika kuhudumia vyema zaidi nchi masikini.
Kadhalika, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Kudhibiti Idadi ya Watu (UNFPA) imetoa mwito maalumu kwa viongozi wa G-8 unaowanasihi wayape umuhimu wa hali ya juu masuala yanayohusu uzazi wa majira, ikijumuisha pia huduma za afya ya mama wajawazito. UNFPA ilikumbusha ya kuwa mahitaji ya dawa za kuzuia mimba yanabashiriwa kuongezeka ulimwenguni kwa asilimia 40 katika miaka 15 ijayo, licha ya kuwa ufadhili wa huduma hizo kimataifa unaendelea kuteremka.