Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAPA NA PALE

HAPA NA PALE

Baraza la Usalama linazingatia ripoti mpya ya KM kuhusu hali katika Afghanistan. Ndani ya ripoti KM amependekeza shughuli za UM ziongezwe katika zile sekta muhimu zenye kuhusu huduma za kufufua uchumi na jamii. Kadhalika KM alitaka idadi ya watumishi wa UM katika Afghanistan iongezwe kwa kima kikubwa zaidi ili kusaidia vyema katika utekelezaji wa miradi yake ndani ya nchi.~~

Shirika la UM juu ya Matumizi ya Amani ya Nishati ya Nyuklia (IAEA) Ijumatano, Julai 09, limeanzisha mazoezi makubwa ya majaribio, ya saa 48, kwenye mitambo ya nishati ya nyuklia iliopo eneo la Laguna Verde, Mexico. Madhumuni ya mazoezi haya ni kupima matayarisho ya aina gani yatahitajika pindi ajali ya nyuklia itachimbuka kwenye mazingira kama hayo katika siku za usoni.

Korti Ndogo ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) imeakhirisha uamuzi wa mahakama ilioendesha kesi wa kumwachia Thomas Lubanga, mtuhumiwa wa makosa ya vita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada ya Mwendesha Mashitaka kuisihi mahakama kwamba si sawa kumwachia huru Lubanga katika nyakati sasa wangali wakisubiri hukumu ya mwisho. Lubanga atasalia kizuizini, chini ya uangalizi wa ICC, mpaka pale Korti ya Rufaa itakapotoa hukumu ya mwisho katika siku zijazo.