Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeanzisha uchunguzi wa awali wa shambulio dhidi ya UNAMID Darfur Kaskazini

UM umeanzisha uchunguzi wa awali wa shambulio dhidi ya UNAMID Darfur Kaskazini

Kwa mujibu wa ripoti za UM, timu ya wanajeshi na polisi wa UNAMID walikwenda kwenye eneo liliopo kilomita 100 kutokea Shangil Tobayi, Darfur Kaskazini kufanya uchunguzi juu ya mauaji ya raia. Walipofika huko walishambuliwa ghafla na wanamgambo wasiotambulikana waliokuwemo ndani ya magari 40 ambayo yalipachikwa bunduki nzito za rasharasha, pamoja na silaha zisiokuwa na vitako na pia silaha za kupiga ndege au eropleni.~~

Taarifa ya UM imesema magari saba ya UNAMID yalichukuliwa na washambuliaji wasiojulikana, na magari mawili mengine yalichomwa moto wakati gari moja liliobeba silaha liliharibiwa kihorera.

Wakati wa mashambulio, walinzi amani wa UNAMID walishiriki kwenye mapigano mazito na makali yaliorushiana risasi kwa muda wa saa tatu mfululizo, hali ambayo ilisababisha vifo na majeruhi mabaya kadha, kwa upande wa askari wa UM.

Uchunguzi wa mwanzo wa UM umeshaanzishwa kwenye lile eneo ambalo mashambulio yalipotukia, kadhia ambayo itafuatiliwa baadaye na uchunguzi rasmi wa tukio hili la kusikitisha dhidi ya walinzi amani wa majeshi mseto ya UM/UA katika Darfur.