Skip to main content

Dokezo ya Ripoti ya KM kuhusu hali katika JKK

Dokezo ya Ripoti ya KM kuhusu hali katika JKK

Wiki hii KM Ban Ki-moon ametoa ripoti maalumu yenye kupendekeza vigezo vya kufikiwa na UM katika kutathminia kama wakati umewadia wa kuanzisha utaratibu wa kuondosha, kwa hatua, vikosi vya ulinzi wa amani vya UM viliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

Kuhusu hali katika jimbo la mashariki, ambalo mara nyingi hupambwa na vurugu, KM alibainisha ndani ya ripoti kwamba mafanikio ya kuleta amani hayatopatikana katika eneo hilo, hususan kwenye utekelezaji wa maafikiano ya amani ya Goma na Nairobi, bila ya kuhusisha kisiasa, na kwa muda mrefu bila ya ubaguzi, makundi yote husika nchini. Aliyahimiza makundi haya kuutumia ule mpango unaojulikana kama Mradi wa Amani, uliobuniwa kutekeleza maafikiano ya karibuni ya Goma na Nairobi, kuwa kama mwongozo wa kujenga hali ya kuaminiana kati yao, na pia aliyataka makundi husika kujaribu kuwasaidia wahamiaji, pamoja na wale raia waliong’olewa makwao na kufanywa wahamiaji wa ndani ya nchi, kukabiliana vyema zaidi na masaibu yaliowakumba kimaisha. Kwa upande mwengine, alisema KM, juu ya kuwa maafikiano ya kusisitisha mapigano yanahishimiwa na kutekelezwa na makundi husika, kwa ujumla, anakhofia hali hiyo huenda isidumishwe kwa sababu ya mapambano yaliojiri karibuni nchini, na kwa kuendelea uandikishaji wa watu wanaojiunga na makundi ya wanamgambo, mambo ambayo KM anahisi yanahatarisha kuchafua na kuzusha, kwa mara nyengine tena, vurugu na fujo katika jimbo la kaskazini-mashariki. Alitaka hali hiyo idhibitiwe haraka kwa kulingana na mapendekezo ya kanuni za kimataifa.