Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon alikuwa mgeni wa hishima mjini Paris kwenye gwaride ilioadhimisha miaka sitini ya operesheni za ulinzi wa amani za UM. Wanajeshi 145 kutoka nchi 25 pamoja na askari wa Kifaransa waliomaliza ulinzi wa amani na vikosi vya UM vya UNIFIL nchini Lebanon walishiriki kwenye gwaride hilo.~~

Ripoti ya KM juu ya hali katika Cote d'Ivoire imepongeza juhudi za makundi husika ya kisiasa na utekelezaji wao mzuri wa mpango wa amani wa Ouagadougou, hususan ridhaa yao ya jumla kuhusu sheria ya kuongoza uchaguzi ujao. Ripoti ilitahadharisha kwamba Cote d'Ivoire bado inakabiliwa na vizingiti kadha wa kadha, ikijumuisha tatizo la masalia ya majeshi ya mgambo, pamoja na upungufu wa fedha za kutayarisha kambi kwa wale wapiganaji wanapokonywa na kusalimisha silaha.

Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO)kwa sasa yanalisaidia taifa la Bukini kukabiliana na mifumko ya Homa ya Bonde la Ufa nchini ambayo huambukiza wanadamu na wanyama wa mifugo, halkadhalika. Mashirika ya FAO na WHO yameshaandaa Mradi wa Dharura kuhudumia wale wenye hatari ya kuambukizwa na maradhi ya Homa ya Bonde la Ufa, mpango ambao utasaidia kuimarisha uangalizi bora, utakuza juhudi za kuripoti haraka magonjwa yakitukia, na pia utaipatia Bukini uwezo wa kupima kwa haraka kwenye maabara yao ubainishaji wa magonjwa.