Skip to main content

Mwendesha Mashitaka wa ICC aomba Mahakama kumshika Raisi wa Sudan

Mwendesha Mashitaka wa ICC aomba Mahakama kumshika Raisi wa Sudan

Luis Moreno-Ocampo Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) Ijumatatu kwenye mji wa Hague, Uholanzi amewakilisha ushahidi ambao anasema unaonyesha Raisi waSudan, Omar Hassan Ahmad Al Bashir alihusika na makosa ya mauaji ya halaiki, jinai dhidi ya utu na makosa ya vita katika jimbo la Darfur, Sudan magharibi.

KM Ban Ki-moon ambaye yupo Ufaransa hivi sasa amenakiliwa, kwa kupitia Msemaji wake, kupokea taarifa yenye kuthibitisha Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) amepeleka ombi la kuwakamata baadhi ya wanajumuiya wa Serikali ya Sudan. KM amesema ana “wasiwasi mkubwa” na mashitaka ya ICC dhidi ya Mkuu wa Taifa la Sudan, na kukhofia athari zake kwa operesheni za ulinzi wa amani ziliopo Sudan kusini na magharibi. KM ametilia mkazo kwenye taarifa yake UM hauna sauti wala uwezo wa kuishawishi Mahakama ya ICC kwenye maamuzi yake, kwa sababu hiyo ni taasisi huru na UM lazima ihishimu uhuru wa utaratibu wa kimahakama. Alisema operesheni muhimu za ulinzi wa amani katika Sudan zitaendelea kuhudumiwa bila ya upendeleo, kwa ushirikiano na makundi yote husika, ili kuimarisha usalama, amani na utulivu nchini. Alitumai Serikali ya Sudan itaendelea kushirikiana kikamilifu na UM kukamilisha majukumu ya kuhakikisha watumishi wa UM na mali zao watalindwa na kuhifadhiwa nchini humo.

Mjumbe wa Kudumu wa Sudan katika UM, Balozi Abdalmahmood Abdalhaleem Mohammad kwenye mahojiano leo asubuhi na Mwandishi wa Redio ya UM Bissera Kostova alisema umauzi wa Mahakama ya ICC kumshika Raisi wa Sudan utawakilisha maendeleo mabaya sana:

"Tunachukulia mashitaka haya kuwa ni maendeleo mabaya sana .. na tunalaani kitendo hiki kwa lugha na kauli nzito kabisa." Alisema kwa maoni ya Sudan kitendo cha Mahakama ya ICC kinachochewa na “mbinu za kisiasa” na angelipendeleea kuona “UM na nchi zote zenye kupendelea amani kusimama imara na Sudan, kwa nguvu moja, kupinga tukio hili hatari.”