Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Serge Brammertz Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Mahakama ya UM juu ya Makosa ya Vita kwa iliokuwa Yugoslavia (ICTR) amewasilisha ripoti maalumu kwa waandishi habari Ijumatatu (21 Julai) ya kupongeza kukamatwa kwa Radovan Karadzic, kiongozi wa kisiasa wa Waserb wa Bosnia na mtoro aliyekimbia adhabu ya sheria kwa muda mrefu katika Bosnia-Herzegovina. Karadzic alishikwa na wenye madaraka Serbia na sasa yupo kizuizini. Karadzic alishitakiwa rasmi na Mahakama ya ICTR miaka 13 iliopita kwa kuongoza makosa dhidi ya utu na mauaji ya halaiki kwa raia wa Bosnia-Herzegovina wasiokuwa Waserb - yaani Wacroat na WaIslamu wa huko. Tutakupatieni taarifa zaidi Ijumanne.

Baraza la UM juu ya Maendeleo ya Uchumi na Jamii (ECOSOC) linakutana Makao Makuu kuzingatia taratibu za kutumiwa kuisaidia UM kukamilisha majukumu yake kwenye shughuli za kudhibiti bora athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

Baraza la Usalama limekutana kwenye kikao cha hadhara kuzingatia operesheni za ulinzi wa amani za shirika la UNMIN katika Nepal. Baada ya hapo kulitarajiwa kufanyika mkutano wa faragha wa kusailia mgogoro uliozuka karibuni katika taifa la Georgia.

Msemaji wa KM ameripoti UM umekubali kujiunga na tume ya maelekezo ya upatanishi kwa Zimbabwe, iliyoundwa na Raisi Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kwa madhumuni ya kusimamia mpango wa kusuluhisha mzozo wa siasa nchini humo. Wajumbe wa tume wanatarajiwa kushauriana, inapohitajika, juu ya namna ya kusukuma mazungumzo ya upatanishi kwa ridhaa y a wopte. Wajumbe wengine waliomo kwenye tume hiyo ni pamoja na wale wanaowakilisha Umoja wa Afrika na vile vile Kitengo cha Masuala ya Siasa, Ulinzi na Amani cha Umoja wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Timu ya wachunguzi wa haki za binadamu wa Shirika la UM la Ulinzi Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (MONUC) imepelekwa kwenye mji wa Mbuji Mayi, katika jimbo la Kasaï Oriental kufanya ukaguzi wa hali za jela zilivyo, baada ya ripoti za kuzidi kwa vifo vya wafungwa kutokana na utapiamlo. Ripoti ya MONUC ilisema tangu tangu Februari 2008 wafungwa 26 walifariki kwa sababu ya utapiamlo mkali. Jengo la jela ya Mbuji Mayo lilipojengwa, MONUC, ilripoti, lilikusudiwa kuwa na wafungwa 200, na jumla ya wafungwa gerezani humo sasa hivi ni sawa na wafungwa 425. Wenye madaraka walikumbushwa dhamana yao ya kuhakikisha hali za jela inaridhisha kwenye magereza yote yaliopo katika nchi.

Kamati ya Majadiliano ya Biashara ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) itakutana kwa wiki nzima Geneva kujadilia masuala kadha ili kuwasilisha mapatano ya mwisho ya Ajenda ya Doha kuhusu Maendeleo, ikijumuisha vile vile masuala yanayoambatana na ruzuku za wakulima na ushuru wa bidhaa, hasa dhidi ya nchi masikini, kwenye soko la kimataifa. Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Shirika la WTO, Pascal Lamy kwenye hotuba ya ufunmguzi aliwaambia wajumbe wa kamati kwamba wako ukingoni wa hatua kuu katika kuikamilisha Duruy a Doha kwa mawaka huu.