HAPA NA PALE

22 Julai 2008

KM ameikaribisha hatua ya utiaji sahihi wa Taarifa ya Mwafaka (MOU) kati ya makundi yaliohasimiana Zimbabwe, kwa matumaini ya kutia moyo, utaratibu ambao umeweka msingi wa makubaliano ya kuanzisha mazungumzo rasmi ya kumaliza mzozo wa kisiasa nchini. KM alimpongeza Raisi Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na timu yake ya wapatanishi kwenye juhudi zao zilizowezesha mwafaka huo kutiwa sahihi. UM upo tayari kusaidia,kwa kila njia, kwenye jitihadi zote za upatanishi nchini Zimbabwe,alisema KM.

Baraza la Usalama Ijumanne linaendelea na mijadala, kwenye kikao cha hadhara kuzingatia hali katika Mashariki ya Kati, ikijumuisha suala la Falastina, na vile vila kujadilia mpango wa amani kwa Nepal. Juu ya Mashariki ya Kati, Naibu KM kuhusua Masuala ya Kisiasa, Lynn Pascoe aliliambia Baraza la Usalama hali ilitia moyo kidogo baada ya mazungumzo ya mzunguko ya upatanishi yanayosimamiwa na Uturuki, kwa niaba ya Israel na Syria, na pia kupunguwa kwa vurugu kwenye Tarafa ya Ghaza. Lakini alisema juuya hayo hali ya wasiwasi bado inaendelea kieneo kutokana na muongezeko wa operesheni za kijeshi kwenye eneo la Magharibi ya Ukingo wa Mto Jordan. Kuhusu Lebanon Pascoe alisema ni ishara nzuri kuona Serikali ya umoja wa taifa ilifanikiwa kuundwa nchini humo.

Kadhalika, KM ametumia salamu za pongezi Dktr. Ram Barana Yadav kwa kuchaguliwa kuwa Raisi wa kwanza wa Jamhuri ya Nepal. Mnamo mwezi Mei Nepal iliamua kuondosha ufalme uliokuwepo nchini kwa miaka 240. KM alitumai makundi yote nchini yatajumuika na kushirikiana kuunda serikali mpya itakayopania kuendeleza zaidi utekelezaji wa mpango wa amani katika Nepal.

Shirika la Vikosi Mseto vya Ulinzi wa Amani vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) limeripoti ya kuwa Ijumatatu alasiri ofisa wa usalama wa cheo cha juu wa UM alishambuliwa kwa kupigwa na wanajeshi wa Serikali ya Sudan katika mji wa El Fasher, na kulazimishwa kupanda gari la kijeshi na baadaye kupelekwa kwenye ofisi ya upelelezi ya jeshi. Ofisa huyo wa UM hivi sasa ameachiwa na amepelekwa hospitali ya UNAMID kufanyiwa matibabu. Kadhalika polisi ya UNAMID imeripoti kuwa imeanzisha doria ya awali ya helikopta iliotumiwa kuchunguza usalama wa zile kambi za wahamaiji wa ndani ya nchi (IDPs). Mjumbe wa Pamoja wa UM/UA kwa Darfur, Rodolphe Adada leo amekutana na Wali (Gavana) wa Darfur Kaskazini, Mohammed Osman Yousif Kibir ambaye alimuahidi Serikali yake itaendelea kuipatia UNAMID ulinzi na hifadhi, kama inavyopaswa, na vile vile kuwapatia msaada kamili na ushirikiano wa kuridhisha kwenye juhudi za kueneza vikosi vya UNAMID na wafanyakazi kieneo.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) ambalo lilisitisha shughuli zake katika baadhi ya sehemu za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa sababu ya ukosefu wa usalama, wiki hii limeanzisha tena huduma za kuwarudisha makwao wale watu waliong’olewa mastakimu kwenye maeneo ya kaskazini. Raia wa Kongo 2,500 walionyimwa mastakimu kutokana na mapigano wanatazamiwa kuvushwa na feri, kwa kupitia Ziwa Albert, na kupelekwa mji wa Gobu, katika jimbo la Ituri.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter