Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kwanza ya mawakili wanawake Usomali kusaidiwa na UNDP

Jumuiya ya kwanza ya mawakili wanawake Usomali kusaidiwa na UNDP

Karibuni, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) limeisaidia Usomali kuanzisha jumuiya ya kwanza ya mawakili wanawake katika jimbo la Somaliland. ~

Taarifa ya UNDP ilibainisha kwamba jumuiya ya mawakili wa kike, ilioanzishwa mapema mwaka huu katika Somaliland, sasa ina wanachama watano, na inatarajia kuongeza wanachama wanawake 17 zaidi, ambao hivi sasa wanamaliza masomo katika Chuo Kikuu cha Hargeisa na watahitimu mwezi Septemba kutoka kitivo cha sheria. UNDP iliwafadhilia wanafunzi hawa wa kike msaada uliowawezesha kuhudhuria masomo yao bila ya matatizo. Kadhalika UNDP iliifadhilia jumuiya ya mawakili wanawake fedha, mafunzo na vifaa vya kuendesha taasisi yao mpya.

UNDP imeripoti kuwa mpaka mwaka jana Somaliland ilikuwa na wakili mwanamke mmoja tu, anayeitwa Ifra Aden Omar, ambaye sasa ndiye mwenye kuongoza jumuiya hiyo ya mawakili wanawake. Mchango aliopokea Bi Omar kutoka UNDP ulimwezesha kutoa msaada nchini, wa sheria, bila malipo, kwa wanawake muhitaji, kadhia aliotumia kuchangia vizuri zaidi katika zile kesi zinazohusu watoto – na wingi wa kesi alizozishughulikia mwanasheria huyo ziliambatana na matatizo ya vurugu za nyumbani, talaka, uingiliaji wa kimabavu, masuala ya kukimu mahitaji ya mtoto, jukumu la kutunza watoto na vile vile urithi.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNDP sasa hivi katika Somaliland bado hakuna mwendesha mashitaka, wala hakimu aliye mwanamke. UNDP inajaribu kushauriana na maofisa wa kizalendo kuhusu nidhamu za kutumiwa ili kuwasaidia wanawake wanaokhitimu sheria kushika madaraka, ama ya mwendesha mashitaka, au kupatiwa mafunzo ziada ya uhakimu.