Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAPA NA PALE

HAPA NA PALE

Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika Cote d’Ivoire (UNOCI) limemaliza kuondosha kituo chake cha mwisho cha uangalizi, katika ile sehemu ya nchi inayojulikana kama Eneo la Msitari wa Kijani, eneo liliotenga sehemu ya kusini, iliokuwa chini ya mikono ya vikosi vya serikali, kutoka ile sehemu ya kaskazini ya nchi, ambayo baadhi ya maeneo yake bado yapo chini ya mamlaka ya waasi wa zamani wa kundi la Force Nouvelles. Eneo la Msitari wa Kijani lenye upana wa kilomita 20 na urefu wa kilomita 600, katikati ya Cote d’Ivoire, ni sehemu ya amani iliowekwa makhsusi, na kudhibitiwa na vikosi vya kimataifa, kwa kulingana na mapatano ya amani ya Ougadouguo, kusaidia kusitisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini na kujenga hali ya kuaminiana miongoni mwa makundi yaliokuwa yakikhasimiana.

Zawadi ya Kimataifa, kwa 2008, kuhusu Ujuzi wa Kusoma na Kuandika, inayotolewa KILA MWAKA na Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) safari hii imetunukiwa mataifa manne wanachama wa UM – Afrika Kusini, Brazil, Ethiopia na Zambia. Zawadi hizi hutolewa kutambua juhudi kubwa za kukuza ilimu ulimwenguni zikichanganyika na zile huduma za marekibisho yenye natija za kitaaluma kwa umma. Kaulimbiu ya mwaka huu ilitilia mkazo zaidi ilimu ya kuamsha hisia kinga dhidi ya janga la UKIMWI, malaria na maradhi ya kifua kikuu, hususan katika mataifa yanayoendelea.