Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Baraza la Usalama linatarajiwa kukutana jioni Makao Makuu kupitisha azimio la kuongeza muda wa operesheni za vikosi vya mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) kufuatilia maridhiano na mataifa ya magaharibi kukubali kuingiza kibwagizo cha pendekezo la nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (UA) kuhusu suala la Mahakama ya ICC ya kutaka kumshitaki Raisi wa Sudan kwa makosa ya jinai ya halaiki katika Darfur. Muda wa awamu iliopita ya shughuli za UNAMID unamalizika saa sita usiku, Alkhamisi, tarehe 31 Julai 2008.~

Kadhalika, UNAMID imeripoti hali ya usalama kwenye maeneo ya operesheni za ulinzi wa amani Darfur zinaendelea kwa utulivu na hali ni shwari. Vikosi vya UNAMID vinafanyisha doria zao katika maeneo yote husika kama kawaida, bila ya matatizo.

Hali kadhalika, Alkhamisi, tarehe 31 Julai (2008) ni siku ya mwisho ya Vitenma kushika madaraka ya Uraisi wa Baraza la Usalama. Kuanzia Ijumaa, 01 Agosti (2008) Ubelgiji itakabidhiwa madaraka ya Uraisi wa duru, na kuongoza shughuli za Baraza la Usalama kwa mwezi Agosti.

Shirika la Kusimamia Ulinzi wa Amani Mipakani Ethiopia/Eritrea (UNMEE) litakomesha operesheni zake zote katika eneo hilo kuanzia saa sita usiku leo Alkhamisi. Kwa mujibu wa ripoti za UNMEE vifaa na mali zote za UM zinazohusiana na huduma za amani mipakanai vitahamishwa kutoka eneo la operesheni zake ndani ya Ethiopia. Wanajeshi pamoja na vifaa vya UNMEE wameshahamishwa kutoka Eritrea baada ya kusitishwa operesheni za kijeshi huko katika Februari 2008, kufuatia ukakamavu wa Eritrea wa kukataa kulipatia Shirika la Ulinzi Amani Mipakani Ethiopia/Eritrea (UNMEE) mafuta ya kuhudumia shughuli zake. Wanajeshi pamoja na watumishi raia wa UM kutoka nchi 46 wameitumikia UNMEE kwa zaidi ya miaka saba. Hivi sasa watu 700 ziada bado wamesalia kutumikia UNMEE - wanajeshi 320 na watumishi raia 130 wanaitumnikia UNMEE katika eneo la mpaka ndani ya Ethiopia, na watumishi raia 250 katika eneo la Eritrea.

Ujumbe maalumu wa uchunguzi, unaongozwa na Idara ya UM juu ya Masuala ya Kisiasa (DPA), unazuru Pembe ya Afrika hivi sasa, kutathminia hali ya kisiasa, usalama na matatizo ya kiutu mipakani kati ya Djibouti na Eritrea, kwa kufuatana na mapendekezo ya KM, baada ya tukio la uhasama liliozuka siku za karibuni kati ya mataifa hayo mawili. Wawakilishi wa Ofisi ya OCHA pamoja na Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM (DPKO) nao vle vile wamejumuika kwenye ziara ya ujumbe wa uchunguzi wa DPA wa kurudisha utulivu na amani katika Pembe ya Afrika.

Christian Balslev-Olesen, Mwakilishi wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) kwa Usomali ameshtumu vikali, na pia kuchukizwa juu ya kuongezeka kwa utumiaji mabavu na vurugu katika maeneo ya kati na kusini katika Usomali, hali ambayo alisema inahatarisha zaidi usalama wa watoto. Alisema UM imepokea ripoti zenye kuonyesha mwaka jana pekee watoto 150 waliuawa na kujeruhiwa kutokana na mashambulio ya kihorera ya mabomu na risasi. Kadhalika, katika wiki iliopita, UM uliarifiwa watoto saba waliuawa baada ya kunaswa kwenye mapigano baina ya vikundi vinavyopinga serikali na vikosi vya Ethiopia: watoto watano waliuawa wakati wanakimbia mapigano wakirejea kutoka skuli, na watoto wawili wengine waliuawa walipokuwa wakicheza mpira kwenye uwanja wa raia. Balslev-Olsen alilaani pia vitendo vya kuajiri watoto wenye umri mdogo kushiriki kwenye mapigano yalioshtadi nchini Usomali.