Skip to main content

Mvua kali na mafuriko yanahatarisha akiba ya chakula Afrika Magharibi: OCHA yahadharisha

Mvua kali na mafuriko yanahatarisha akiba ya chakula Afrika Magharibi: OCHA yahadharisha

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba nchi kadha za Afrika Magharibi zimeathirika na uharibifu unaochochewa na mfululizo wa mvua kali zilizonyesha huko katika siku za karibuni, hususan katika mataifa ya Burkina Faso, Mali na Togo.

"Nilihadharishwa hii leo asubuhi kuhusu hali katika Togo, ambako, kutokana na makadirio ya Shrikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Vyama vya Hilali Nyekundu (IFRC) watu 10,000

wakiwemo wanawake 6,000 na watoto 2,000

wameshaathirika na hali hiyo, na wakati huo huo nyumba 400 ziada ziliangamizwa, madaraja 9 yameharibiwa, ikiwemo lile daraja linalounganisha Togo na Burkina Faso, hali ambayo, kwa ujumla, imesitisha na kuchafua biashara ya eneo hilo." Alisema maafa haya yamesababisha mzozo wa chakula kuibuka kwenye sehemu ziliopo mbali na palipoharibiwa madaraja, maeneo yenye kutegemea miundombinu hiyo ya usafiri kuvusha bidhaa za chakula. Kadhalika katika Mali, alisema ofisa wa OCHA, mafuriko huko yalisababisha vifo vya watu 6, na anakadiria idadi ya waathiriwa wa maafa itaongezeka baada ya taarifa kukamilishwa kuhusu hali kwenye mataifa ya Cote d’Ivoire na Mali. Alikumbusha kwamba msimu wa mvua katika Afrika Magharibi, kwa sasa umeshakamilisha nusu tu ya majira ya mvua, na makadirio ya UM ni kwamba watu 50,000 wameshathirika sasa hivi na inakhofiwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kuanzia kati ya mwezi Agosti mpaka kati ya Septemba kwa sababu wakati huo ndio mvua kali sana huteremka kwenye eneo.