Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'UM uliopoa' kutunza mazingira Makao Makuu

'UM uliopoa' kutunza mazingira Makao Makuu

Kuanzia Ijumaa tarehe mosi Agosti, UM utatekeleza mradi maalumu kwenye majengo ya Makao Makuu yaliopo New York, kwa matarajio ya kuongeza akiba ya fedha za matumizi na kutunza mazingira. Hatua hii inachukuliwa kwa kulingana na juhudi za kimataifa za kukabiliana na matatizo yanayotokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, na UM imeamua kuongoza kwenye juhudi hizi kwa vitendo.

Mradi mpya wa UM utakuwa ni wa majaribio, na unajulikana kama "Mradi wa UM Iliopoa" kwa maana vifaa vya kurekibisha joto katika Makao Makuu vitaongeza halijoto kwenye majengo yake kutoka nyuzijoto 72 hadi 75 za Fahranhaiti. Mnamo mwisho wa wiki virekibisha joto vitazimwa kabisa. Shughuli hizi zinatazamiwa kupunguza tani 300 za hewa chafu inayomwagwa angani na UM, punguzo la asilimia 10 ya nishati inayotumiwa na vifaa vya kupooza joto. Kadhalika, UM utafaidika kwa huduma hizi na kuongeza akiba ya dola 100,000 ziada, gharama za mvuke unaohudumia shughuli hizo. Vile vile watumishi wa UM walinasihiwa na KM kuvaa nguo za kawaida wanapokuja kazini katika mwezi wa Agosti, badala ya kuvaa mavazi rasmi, yanayojumuisha suti na tai na kadhalika.