Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa FAO, Papa Benedict XVI na Brazil wanatathminia mzozo wa chakula duniani

Mkuu wa FAO, Papa Benedict XVI na Brazil wanatathminia mzozo wa chakula duniani

Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO), taasisi inayosimamia shughuli za mkutano wa kuzingatia mgogoro wa chakula duniani, kwenye hotuba yake alitilia mkazo kwamba tatizo la njaa ulimwenguni linaweza kusuluhishwa kwa urahisi, na haraka zaidi, pindi jumuiya ya kimataifa itaweza kuchangisha, kila mwaka dola bilioni 30. Alishtumu na kusikitika kwamba jamii ya kimataifa hupoteza dola bilioni 1,200 kila mwaka kwenye silaha, wakati katika kipindi hicho hicho thamani ya chakula cha dola bilioni 100 huangamizwa na taifa moja tajiri pekee, na huku wale watu wanene na watipwatipwa huonekana wakiteketeza chakula kinachogharamiwa dola bilioni 20 kila mwaka.

Kadhalika, Papa Benedict wa XVI kwenye salamu zake zilizowasilishwa mkutanoni alikariri pia kwamba “njaa na utapia mlo ni matatizo yasiokubalika asilan kimaadili, hasa katika mazingira ya ulimwengu uliojaaliwa, sio uwezo maridhawa pekee wa kukomesha haraka athari na msiba wa njaa bali pia umejaaliwa ujuzi wa kisasa wa kukomesha matatizo ya chakula kikamilifu.”

Lakini Raisi wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva yeye kwenye risala yake alitetea haki ya taifa lake kutumia nishati ya viumbehai, inayozalishwa na mazao ya nafaka, kadhia ambayo alisisitiza ni “chombo muhimu dhidi ya matatizo ya njaa na chakula” pindi mradi husika utadhibitiwa kwa uangalifu unaofaa.