Skip to main content

Mukhtasari wa Mkutano wa UM Kudhibiti Akiba ya Chakula Duniani

Mukhtasari wa Mkutano wa UM Kudhibiti Akiba ya Chakula Duniani

Mkutano Mkuu wa UM kuhusu Udhibiti Bora wa Akiba ya Chakula Duniani ulitarajiwa kukamilisha mijadala yake mjini Roma Alkhamisi ya leo na kuwasilisha taarifa ya mwisho ambayo, nilipoelekea studio ilikuwa bado haijapitishwa. Taarifa hiyo ilisubiri uamuzi wa mataifa ya Amerika ya Latina kuhusu matumizi ya nishati inayozalishwa na mavuno ya nafaka, kadhia ambayo hudaiwa ndio inayochochea mifumko ya kupanda kwa kasi bei za chakula na kuongeza athari haribifu katika mazingira.~

Halkadhalika, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kwamba litanunua chakula kwa wingi zaidi katika mataifa yanayoendelea, ili kukuza uchumi wao.

Ijumatano mjjini Roma mashirika matatu ya UM yanayohusika na shughuli za chakula na kilimo, yaani FAO, IFAD na WFP yalitia sahihi Hati ya Mwafaka, na Jumuiya ya Ushirikiano wa Mapinduzi ya Kilimo Afrika (AGRA), makubaliano yenye lengo la kukuza ushirikiano katika kuzalisha chakula kwenye yale maeneo ya Afrika yenye rutuba, yanayojulikana kama “kanda za vikapu vya mikate”, huduma ambayo inatarajiwa itawasaidia zaidi kiuchumi wale wakulima wadogo wadogo. Mwenyekiti wa Jumuiya ya AGRA ni KM Mstaafu Kofi Annan.