Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti juu ya juhudi za kufufua nafasi za elimu mitaani Kenya

Ripoti juu ya juhudi za kufufua nafasi za elimu mitaani Kenya

Wiki hii tuna ripoti kuhusu juhudi za kufufua huduma za elimu ya msingi katika Kenya, ambazo ziliharibiwa na machafuko yaliotukia nchini humo kufuatia uchaguzi wa mwisho wa 2007.~

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) vurugu lililoivaa Kenya baada ya uchaguzi kumalizika, lilisababisha vifo vya watu 1,000 ziada na watu 300,000 wengine walilazimika kuhama makwao ili kunusuru maisha. Ama kwa wale watoto waliokuwa wakihudhuria skuli za praimari, uhamisho huo ulizusha hali ya wasiwasi kwao na iliwasilisha maafa kadha wa kadha yalioathiri usalama na hata kuwanyima watoto hawo uwezo wa kuhudhuria skuli kupata masomo yanayolingana na umri wao. Hapa inafaa ikumbukwe ya kuwa watoto wanaotoka kwenye mazingira ya hali duni na ufuakara, mara nyingi hutumia mazingira ya skuli kuwa ni mahali pa kupata hifadhi na usalama.

Mwandishi habari aliyeajiriwa na Redio ya UM nchini Kenya, Ann Weru alipata fursa ya kuzuru mtaa wa mabanda wa Kibera, kitongoji cha mji wa Nairobi, kilichoathirika kihali na mali, kufuatia machafuko yaliozuka mwisho wa 2007 kutokana na ubishani wa matokeo ya uchaguzi nchini. Ifuatayo ni ripoti ya Ann akielezea hali halisi ilivyo Kibera kwa sasa katika sekta ya elimu.

Sikiliza ripoti kamili kwenye idhaa ya mtandao