Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati umewadia kukomesha kwa vitendo utumiaji mabavu dhidi ya Wanawake

Wakati umewadia kukomesha kwa vitendo utumiaji mabavu dhidi ya Wanawake

Wiki hii Naibu KM Asha-Rose Migiro alipata fursa ya kuzungumzia suala la udhalilishaji wa kijinsia, kwenye mkutano maalumu uliotayarishwa mjini New York na Halmashauri ya Mataifa ya Ulaya pamoja na Ubalozi wa San Marino katika UM. Kwenye risala alioitoa mbele ya kikao hicho NKM Migiro alihimiza kuchukuliwe hatua za pamoja, kukomesha haraka tabia ya utumiaji nguvu na mabavu dhidi ya wanawake, hatua ambayo ikikamilishwa, alitilia mkazo, itawavua wanawake na mateso hayo maututi.~

Juhudi za UM katika kupambana na ukatili wa kijinsia, alisisitiza NKM, "zinapiga hatua ya kasi" kimataifa. Kuthibitisha hayo, alitoa mfano juu ya namna Mfuko wa Kimataifa Kukomesha Utumiaji Mabavu dhidi ya Wanawake unavyoendelea kupokea misaada ya fedha, kwa wingi, kutoka wahisani wa kimataifa. Hata hivyo alisema lengo hasa la UM ni kuhakikisha wahisani wa kimataifa watachangia, kwa wastani, dola milioni 100 kila mwaka kudhibiti tatizo la utumiaji mabavu wa kutesa wanawake, kuanzia mwaka huu hadi tutakapofika 2015.

NKM Asha-Rose Migiro pia ameyahimiza mashirika ya kikanda kusaidiana kuratibu sheria za pamoja, zilizo madhubuti, zenye uwezo wa kuwalinda wanawake na makosa ya kijinsia na pia kuwapatia hifadhi ya kisheria itakayohakikisha wanaume wanaoshiriki kwenye vitendo vya kutumia mabavu ya kutesa wanawake wataadhibiwa.