Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mukhtasari wa Mkutano Mkuu wa UM Kuzingatia Juhudi za Kudhibiti UKIMWI Duniani

Mukhtasari wa Mkutano Mkuu wa UM Kuzingatia Juhudi za Kudhibiti UKIMWI Duniani

Mkutano dhidi ya UKIMWI ulifanyika kwenye Makao Makuu ya UM mjini New York, kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni 2008, ambapo mijadala ya wawakilishi wote iliendelezwa na kushtadi kwenye ukumbi wa Baraza Kuu. Mkutano Mkuu ulikusanyisha Raisi wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim, KM wa UM Ban Ki-moon na Wakuu kadha wa Mataifa pamoja na mawaziri zaidi ya 80, na pia maofisa wa vyeo vya juu wa UM na mashirika yake kadha wa kadha, na vile vile wawakilishi wa taasisi za kimataifa na jumuiya za kiraia.

Kwenye hotuba ya ufunguzi wa kikao cha wawakilishi wote mbele ya Baraza Kuu, KM wa UM Ban Ki-moon aliyapongeza "mafanikio muhimu" yaliofikiwa na Serikali za kimataifa katika kuwapatia raia uwezo wa kujikinga na hatari ya kupatwa na virusi vya UKIMWI itakapofika 2010, na vile vile kufadhilia misaada na uangalizi unaofaa kiafya kwa raia wagonjwa wa maradhi husika. KM aliuhimiza umma wa kimataifa kuachana na tabia karaha ya kubagua na kuwatenga watu walioambukizwa na virusi vya UKIMWI, kwa sababu, alionya, kitendo hicho ni "tusi na kashfa kuu isiolingana na utu wetu wa pamoja."

KM aliwasilisha mkutanoni ripoti maalumu iliofanyia tathmini ya juhudi za kimataifa katika kuyafikia yale malengo ya kudhibiti bora matatizo ya UKIMWI/VVU. Ripoti iyo ilidhihirisha kwamba kumepatikana mwelekeo wa kutia moyo kwenye bidii hizo, hasa katika zile huduma za kuwapatia tiba inayofaa akina mama wajawazito wenye vijidudu vya UKIMWI, matibabu ambayo husaidia kuwapatia watoto wachanga kinga dhidi ya maambukizo ya madhara ya virusi vya mama.

Dktr Peter Piot, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Pamoja wa Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI/VVU (UNAIDS) – ambaye alizungumzia kwa mara ya mwisho kama kiongozi wa taasisi hiyo – alitahadharisha kwenye risala yake ya kuwa si haki kwa Mataifa Wanachama kuweka vikwazo dhidi ya watu wanaoishi na UKIMWI kuingia kwenye maeneo yao. Dktr Piot alipendekeza tabia hii ikomeshwe haraka; na vile vile alisema wakati umeshawadia, kuchukua hatua halisi za kuwatetea, hadharani, wanawake, kwa ujumla, na kukabiliana na ubaguzi wa kijinsiya na madhila dhidi ya wanawake. Kadhalika alinasihi watu kukomesha hofu zao za wasenge pamoja na tabia nyenginezo zenye kukiuka haki za binadamu, tabia ambazo, alitahadharisha, kama hazijakomeshwa, zitaenedelea kutatanisha juhudi za kimataifa za kupambana kikamilifu na janga la UKIMWI.

Dktr Piot pia alikumbusha ya kwamba licha ya kuwa kumepatikana mafanikio muhimu, na ya kutia moyo hivi karibuni, katika kupiga vita UKIMWI, hata hivyo tusisahau kwamba VVU bado vinaendelea kusumbua na kusababisha vifo vya watu 6,000 kila siku duniani; na katika bara la Afrika VVU ndio chanzo cha awali chenye kusababisha vifo vya raia, ambavyo idadi yake imepindukia ile jumla ya vifo vinavyotokana na malaria. Alisema takwimu za utafiti wa UM zimebainisha ya kuwa katika kila wagonjwa wawili wanaoishi na virusi vya UKIMWI, wanaohudumiwa zile dawa za kurefusha maisha, kuna watu watano wengine wanaoambukizwa na vijidudu hivyo. Dktr aliitahadharisha jumuiya ya kimataifa ya kwamba hali hii inahitajiwa kudhibitiwa kidharura, kabla haijaangamiza mafanikio yaliofikiwa siku za nyuma kwenye juhudi za kupambana na UKIMWI.

Raisi wa Baraza Kuu la UM, Srgjan Kerim ambaye aliongoza mijadala ya siku tatu hapa Makao Makuu, yeye katika risala yake alionya kwamba pindi walimwengu watashindwa kufanya maendeleo katika kudhibiti bora, kipamoja, tatizo la UKIMWI/VVU hali hiyo anakhofia itaathiri vibaya huduma zote za maendeleo, mathalan, zile shughuli za kupunguza njaa, hasa katika kilimo, ambazo zitapwelewa kwa sababu mamilioni ya watu wanaohudumia sekta hiyo ya kilimo wameonekana kufariki wangali bado wana umri wenye uwezo wa kufaidisha jamii zao, na vile vile sekta ya elimu huenda ikaharibiwa kwa sababu imedhihirika idadi kubwa ya walimu hufariki kimataifa, kushinda ile jumla ya watu wanaohitimu mafunzo ya ualimu .

Katika hotuba ya kufunga mijadala hapo Alkhamisi magharibi Raisi wa Baraza Kuu, Srgjan Kerim alizihimiza Serikali Wanachanma na viongozi wa kitaifa na kimataifa, kuimarisha huduma za afya na kukuza ile miradi ya kupambana na maradhi ya UKIMWI, kipamoja, ili kujikwamua, kwa nguvu moja, kutokana na janga maututi la UKIMWI.